CONAKRY: Watu 12 wauawa katika ghasia nchini Guinea
11 Februari 2007Si chini ya watu 12 wameuawa katika ghasia zilizotokea nchini Guinea,huku vyama vya wafanyakazi vikiapa kuendelea na mgomo wa kazi.Machafuko yalizuka,baada ya Rais Lansana Conte kumtangaza Eugene Camara kama waziri mkuu mpya. Hapo awali,mashahidi walisema kuwa vijana watatu waliokuwa wakipinga kuchaguliwa kwa Camara, walipigwa risasi na wanajeshi ukingoni mwa mji mkuu Conakry.Na katika mji wa Kankan ulio mashariki mwa nchi,mwanajeshi mmoja alipigwa na kundi zima,na kiwiliwili chake kikachomwa moto na umati uliohamaki.Wapinzani wa Conte wanasema, mwandamizi wa chama alietangazwa kushika wadhifa wa waziri mkuu,yuko karibu mno na ukoo wa rais, kuweza kuwa mtu anaeaminika kuongoza serikali. Vyama vya wafanyakazi ambavyo vinasema,Rais Conte hafai tena kutawala,baada ya kuwa madarakani miaka 23,wamempa rais huyo hadi Jumatatu kumteua waziri mkuu mpya,kama alivyokubali majuma mawili ya nyuma,ili kumaliza mgomo wa taifa wa siku 18 uliopelekea kuuawa kwa watu 90.