1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cologne na Dortmund zaendelea kuyumba

11 Desemba 2017

Viongozi wa Bundesliga Bayern Munich wana kila sababu ya kufurahishwa na kazi yao wakati wakiingia katika michuano ya katikati ya wiki, baada ya kuimarisha uongozi wao kileleni Bundesliga

https://p.dw.com/p/2p9mS
1. Bundesliga 15. Spieltag | Borussia Dortmund - Werder Bremen
Picha: Reuters/T. Schmuelgen

Washika mkia Cologne hawajapata ushindi wowote msimu huu na wanalenga kusahau kile kocha Stefan Ruthenbeck alielezea kuwa ni hali "yenye uchungu” hapo jana, wakati walipofungwa mabao manne kwa matatu na washika mkia wenzao Freiburg, hata wakati walikuwa wanaongoza kwa mabao matatu kwa bila kwenye mchezo huo. Cologne watacheza dhidi ya Bayern Munich siku ya Jumatano. Bayern wanaongoza msimamo wa ligi na pengo la pointi nane kufuatia ushindi wa moja bila dhidi ya Eintracht Frankfurt. "Pongezi kwa timu. Tulifanya kile tulipaswa kukifanya. Timu ilianza kwa kasi sana na tulipambana kwelikweli na kuonesha kandanda zuri. Tulicheza vizuri kwa dakika 90 na hivyo nivdyo tulitaka kufanya. Na kwa Bayern kupata ushindi wa moja bila kupitia nafasi moja tu, hilo linaweza kutokea

Borussia Dortmund - Vorstellung Peter Stöger, neuer Trainer
Stoeger ana kibarua katika BVBPicha: Getty Images/Bongarts/C. Koepsel

Kocha wa zamani wa Cologne Peter Stoeger alipewa jana majukumu ya kuliokoa jahazi la Borussia Dortmund na kazi yake ya kwanza itakuwa mchuano mkali ugenini dhidi ya Main hapo kesho Jumanne. Dortmund wako katika nafasi ya nane na wameshinda moja tu kati ya mechi 13 zilizopita katika mashindano yote chini ya kocha aliyetimuliwa jana Peter Bosz. Dortmund ilizabwa na Werder Bremen mabao mawili kwa moja katika mechi ya mwisho ya Bosz ambaye alisema vijana wake hawakujiamini "Leo nadhani pia hatukucheza vizuri kiakili, hasa katika kipindi cha kwanza. Hii haimaanishi tu katika mapambano, lakini pia jinsi tulivyoshambulia na tulivyocheza katika ulinzi. Hivyo basi unawapa jukumu wachezaji wengine. Tunapaswa kuwa na wasiwasi kuhusu hilo kwa sababu sio vizuri".

Mainz wako katika nafasi ya 14 juu ya Cologne katika eneo la kushushwa ngazi. Ni pointi nne tu zinazotenganisha Wolfsburg katika nafasi ya 11 na nambari mbili kutoka mkiani Werder Bremen, ambao watashuka dimbani na Bayer Leverkusen siku ya Jumatano.

1. Bundesliga 15. Spieltag | Borussia Dortmund - Werder Bremen | Peter Bosz
Bosz aliamua kusalimu amriPicha: picture-alliance/dpa/I. Fassbender

Wolfsburg itacheza kesho dhidi ya RB Leipzig kabla ya Freiburg kuwaalika Borussia Moenchengladbach. Gladbach ilibakia katika nafasi ya nne, baada ya kutoka sare ya bao moja kwa moja na nambari tatu Schalke siku ya Jumamosi. Christopher Kramer ni kiungo mkabaji wa Gladbach "Nnaweza tena kukasirishwa kwa karibu nusu siku na mwamuzi msaidizi anayetumia video kwa sababu ukitazama dakika mbili kabla ya uamuzi wake muhimu, utapata kitu. Kama tungepewa penalti au kufunga wakati shuti iliupiga mlingoti huo ni wakati mzuri kisaikolojia kufanya mambo yawe 2-0. Tunakubali pointi moja lakini tulistahili zaidi ya hiyo".

Katika mechi nyingine, nambari 15 kwenye ligi SV Hamburg watachuana na Eintracht Frankfurt. Hoffenheim watawaalika VfB Stuttgart, Hertha Berlin dhidi ya Hanover na Schalke watafunga kazi dhidi ya  Augsburg.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/AP/DPA/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman