Clinton barani Afrika.
12 Agosti 2009Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton ameitaka Nigeria iwe na msimamo thabiti katika kupambana na rushwa na ameahidi msaada ili kuunga mkono juhudi za kuleta mageuzi katika mfumo wa uchaguzi.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi habari pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Nigeria ,waziri Clinton amesema leo mjini Abuja kuwa nchi yake inaunga mkono thabiti juhudi za serikali ya Nigeria za kuleta uwazi zaidi, na kupunguza rushwa .
Waziri Clinton pia amesema kuwa Marekani ipo tayari kusaidia katika kuanzisha michakato ya demokrasia ikiwa ni sehemu ya matayarisho ya uchaguzi utakaofanyika mwaka 2011.
Rushwa pamoja na usimamizi mbaya wa raslimali vimekwamisha maendeleo, vitega uchumi ,vimehujumu demokrasia na kusababisha migogoro katika jimbo la Niger Delta na mvutano wa kidini kaskazini mwa Nigeria.
Akijibu kauli ya waziri Clinton ,waziri wa mambo ya nje wa Nigeria bwana Ojo Maduekwe amesema kuwa, nchi yake inatambua kwamba kukosolewa hakuna maana ya kukasirishwa ama kuchochea mabaya.
Waziri Maduekwe pia amesema anatambua kwamba wanaoikosoa Nigeria wanaitakia mema. Hatahivyo amesema serikali ya Nigeria imezingatia wasiwasi na yaliyosemwa na rafiki.
Katika ziara yake ya nchi kadhaa barani Afrika waziri wa mambo ya nje wa Marekani Clinton amekuwa anasisitiza ujumbe juu ya kupambana na rushwa Katika ziara yake nchini Nigeria waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton pia atakutana na rais Umaru Yar'Adua. Kesho ataelekea Liberia.