Clinton yuko Oman kujadili mageuzi
19 Oktoba 2011Clinton kwanza atamshukuru Sultan Qaboos kwa kusaidia kuachiliwa na Iran hapo mwezi uliopita kwa wapanda milima wa Marekani Josh Fattal na Shane Bauer ambao walikuwa wakishikiliwa nchini Iran baada ya kukamatwa karibu na mpaka wa Iran na Iraq hapo mwaka 2009.
Wamarekani hao wawili walikamatwa pamoja na mwenzao mwengine mpanda milima wa Marekani Sarah Shourd,ambaye aliondoka Iran hapo mwezi wa Septemba mwaka jana baada ya kuachiliwa kwa dhamana kwa misingi ya kibinadamu na matibabu.
Kama vile ilivyokuwa kwa wenzake wawili dhamana ya Shourd ilikuwa ni dola 500,000 na zililipwa kwa kupitia Oman, mshirika wa Marekani katika eneo la nchi za Ghuba ambayo anaendelea kuwa na uhusiano wa kirafiki na Iran.
Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani akizungumza na waandishi wa habari akiwa safarini kuelekea Muscat mji mkuu wa Oman amesema Clinton katika ziara yake hiyo pia atafuatilia mazungumzo yake na Mfalme Qaboos yaliofanyika nchini Oman hapo mwezi wa Januari kuhusu mageuzi ya kijamii na kiuchumi halikadhalika masuala ya maendeleo na elimu nchini humo.
Hapo Jumamosi iliopita Oman ilipiga kura kulichagua baraza lao la ushauri Majlis al- Shura ambalo Sultan Qaboos ameahidi kulipa madaraka mapya kutokana na kuzuka kwa machafuko ya kijamii ambayo hayajawahi kushuhudiwa kabla nchini Oman.
Wanaharakati watatu ambao walishiriki katika maandamano nchini Oman mapema mwaka huu walichaguliwa katika baraza hilo lenye wajumbe 84 na kuleta matumaini kwamba wito wa mageuzi utaitikiwa na baraza hilo lililongezewa madaraka.
Sultan Qaboos bin Said aliempinduwa baba yake hapo mwaka 1970 alikabiliana na machafuko ya mwezi wa Februari kwa ahadi za kufanya mageuzi na kutowa misaada ya fedha pamoja na kulipa baraza hilo baadhi ya madaraka ya kisheria na kikanuni kwa mara ya kwanza kabisa.
Watu watano waliuwawa katika maandamano ya mwezi wa Februari ambayo yalizuka katika mji wenye viwanda wa Sohar nchini Oman na yalikuja kufuatia machafuko ya Misri na Tunisia. Vijana wengi walioandamana wakati huo walidai kuongezewa mishahara na kukomeshwa kwa rushwa nchini Oman.
Inaelezwa kwamba Clinton pia atamtahadharisha Sultan Qaboos juu ya machafuko ya umwagaji damu yanayoendelea katika nchi za Kiarabu za Syria na Yemen ambapo watawala madikteta wamekuwa wakitumia nguvu kubwa dhidi ya vuguvugu la kudai demokrasia.Yemen ni nchi jirani na Oman.
Clinton pia anatazamiwa kuitumia ziara hiyo kuelezea wasi wasi wa Marekani juu ya tabia ya Iran hususan madai ya njama ya Iran iliotangazwa na maafisa wa Marekani wiki iliopita ya kumuuwa balozi wa Saudi Arabia mjini Washington.
Afisa wa wizara ya mambo ya nje wa Marekani amewaambia waandishi wa habari kwamba wangelitaraji Waomani watautumia uhusiano wao na Iran kama walivyofanya huko nyuma kuwasaidia Wairan kufahamu athari ya kile wanachokifanya.
Clinton amewasili Oman baada ya kufaya ziara fupi nchini Malta na Libya ambapo alitaka kuendelezwa kwa mchakato wa kidemokrasia wa kipindi cha mpito na upinzani iliompinduwa Kanali Muammar Gaddafi hapo mwezi wa Augusti.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP/RTRE
Mhariri:Yusuf Saumu