1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton, Trump waongoza uchaguzi wa Jumanne Kabambe

Grace Patricia Kabogo2 Machi 2016

Hillary Clinton wa chama cha Democratic na Donald Trump wa Republican wanaongoza katika uchaguzi wa mchujo wa kuwateua wagombea urais Marekani, unaojulikana kama Super Tuesday yaani Jumanne Kabambe.

https://p.dw.com/p/1I5FV
Picha: picture-alliance/dpa/AP Photo/C. Kaster

Baada ya wananchi wa Marekani kupiga kura hapo jana kwenye majimbo 11, mgombea wa Democratic, Hillary Clinton ameshinda katika majimbo ya Virginia na Georgia baada ya kupata kura 45, dhidi ya mpinzani wake Bernie Sanders, aliyepata kura 30. Aidha Sanders ameshinda katika jimbo la Vermont na Oklahoma.

Akizungumza baada ya ushindi wa Vermont, Mdemocrat, Sanders, amesema kampeni ni kuhusu mabadiliko nchini Marekani na mapinduzi ya kisiasa na sio tu kumchagua rais.

Clinton ameshinda pia katika majimbo ya Alabama, Texas, Massachussets na Tennessee. Aidha, ameshinda kwenye jimbo la Arkansas, jimbo ambalo mume wake, Bill Clinton alilitumikia akiwa gavana.

Mrepublican Donald Trump, ameshinda katika jimbo la Georgia. Baada ya kuwashinda wapinzani wake Marco Rubio, Ted Cruz na John Kasich, bilionea huyo aliandika katika mtandao wake wa kijamii wa Twitter akisema ''Asante Georgia!''

Trump ameshinda pia katika majimbo ya Virginia, Massachusetts, Alabama, Tennessee na Arkansas. Utafiti wa maoni baada ya kupiga kura unaonyesha kuwa Trump na Kasich wanachuana vikali katika jimbo la Vermont. Mpinzani wa Trump, Seneta Cruz ameshinda katika majimbo ya Texas na Oklahoma.

Cruz awataka wagombea wa Republican kuungana dhidi ya Trump

Kwa upande wa majimbo ya Colorado na Minnesota, Barnie Sanders ameshinda kwa upande wa chama cha Democrats, huku Marco Rubio akilinyakua jimbo la Minnesota kwa upande wa Warepublican. Cruz amewaambia wagombea wa Republican ambao hawajashinda hata jimbo moja, waungane dhidi ya Trump.

Utafiti wa maoni uliofanywa na kituo cha utafiti cha Edison unaonyesha kuwa majimbo manane kati ya tisa, wapiga kura wa chama cha Democratic wanataka muendelezo wa sera za Rais Barack Obama. Kiasi ya theluthi moja ya wapiga kura wamesema wanataka hata sera zaidi za kiliberali. Wapiga kura wa Republican wameelezea kuikataa serikali ya shirikisho.

Ted Cruz wa chama cha Republican
Ted Cruz wa chama cha RepublicanPicha: Getty Images/E. Schlegel

Aidha, utafiti wa kituo cha televisheni cha Marekani, CNN umeonyesha kuwa wagombea wote wa chama cha Democratic, Hillary Clinton na Bernie Sanders, wanaweza wakamuangusha Trump, iwapo uchaguzi mkuu wa Novemba 8, ungefanyika sasa.

Warepublican wanahitaji kupata angalau wajumbe 1,237 na Wademocrats wajumbe 2,383. Hadi sasa Clinton amepata jumla ya wajumbe 337, huku Trump akiwa na wajumbe 182. Sanders amepata wajumbe 191.

Rais Obama anatarajiwa kuondoka madarakani mwezi Januari mwaka ujao, kwa mujibu wa katiba ya Marekani inayokataza kiongozi kukaa madarakani kwa zaidi ya mihula miwili ya miaka minne minne.

Wakati huo huo, kesi iliyofunguliwa dhidi ya mgombea wa kuwania nafasi ya urais kwa chama cha Republican, Seneta Ted Cruz, kupinga uhalali wake kugombea urais wa Marekani, imetupiliwa mbali na Jaji wa Illinois, Maureen Ward Kirby.

Kesi hiyo ni ya madai kwamba Cruz hawezi kugombea kwa sababu ni mzaliwa wa Canada. Kulingana na katiba ya Marekani, mgombea urais anapaswa kuwa mwenye asili ya uraia wa Marekani.

Matokeo kutoka kwenye majimbo yaliyosalia yanatarajiwa kutolewa katika muda wa saa chache zijazo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP,RTR, AP,DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman