Clinton azindua dawa ya bei nafuu kupambana na malaria Tanzania
23 Julai 2007
Mradi uliozinduliwa na rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, unalenga kuwepo kwa dawa ya ACT, mchanganyiko wa dawa mbalimbali itakayoyaokoa maisha ya wengi. Dawa hiyo itauzwa kwa bei ya asilimia 90 chini ya bei ya sasa kwa muuzaji mkubwa wa kitaifa atakayeisambaza katika maduka ya mikoani.
Ugonjwa wa malaria huua watu takriban milioni tatu kila mwaka duniani kote na kuwafanya wengine kiasi ya milioni 300 kuwa wagonjwa sana. Asilimia 90 ya vifo hivyo hutokea barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara, hususan miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano.
Maisha ya wengi yanaweza kuokolewa kutumia mchanganyiko wa dawa ya ACT ambayo ni bora zaidi katika kutibu malaria ikilinganishwa na dawa nyingine ambazo zimekuwa zikitumiwa kutibu malaria kama vile chloroquine. Lakini bei ya kati ya dola nane na kumi inazifanya dawa hizo kuwa ghali mno kiasi cha watu kutoweza kuzimudu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika kitongoji cha Pugu Kajiungeni, nje ya jiji la Dar es Salaam jana baada ya kuzuru maduka matatu ya dawa, Bill Clinton alisema hakuna mtu anayetakiwa kufariki dunia kutokana na ugonjwa wa malaria.
Ingawa kampuni zinazotengeneza dawa kama vile Norvatis na Sanofi Aventis zimepunguza bei ya dawa ya ACT kufikia kiwango cha dola moja inapotumiwa katika sekta ya umma, Waafrika wengi hawawezi kumudu bei hiyo kwani hununua dawa kibinafsi.
Nchini Tanzania takriban nusu ya wagonjwa wa malaria hutafuta matibabu kupitia maduka ya kibinafsi ya kuuza dawa, badala ya taasisi za umma za afya na wengi wao hawawezi kumudu bei ya dawa hizo za ACT. Badala yake hununua dawa za zamani ambazo bei yake ni kati ya mara 20 hadi 30 rahisi kuliko bei za dawa ya ACT lakini mara nyingi haziponyi malaria kwa sababu ya usugu wa dawa.
Mradi uliozinduliwa na wakfu wa Clinton unalenga kujaribu uwezo wa kupunguza bei ya dawa za ACT kama njia ya kuongeza matumizi yake. Mradi huo utatekelezwa katika maeneo mawili katikati mwa Tanzania na unalenga watu 450,000 kila mwaka.
Dawa ya ACT hutengenezwa kutokana na mmea unaokuzwa nchini China na utengenezaji wake una gharama kubwa. Mashirika ya kimataifa na serikali, zikiwemo Uholanzi na Uingerza, zinatafakari juu ya mpango wa kimataifa wa kupunguza bei ya dawa ya ACT, utakaogharimu mamilioni ya dola.
Clinton akiwa katika ziara ya nchi nne barani Afrika, zikiwemo Afrika Kusini, Malawi, Zambia na Tanzania, alisema wakati alipokutana na rais Levy Mwanawasa wa Zambia kwamba wakfu wake utasaidia kutoa mafunzo kwa wataalam wa afya nchini humo kuenzi juhudi za Zambia katika vita dhidi ya ukimwi.