Clinton ashinda South Carolina kabla ya "Jumanne kuu"
28 Februari 2016Na ushindi huo unamwelekeza katika siku muhimu wiki ijayo , ijulikanayo kama "Jumanne kuu" ambapo majimbo 11 yatapiga kura.
Ushindi huo unaimarisha hadhi ya Clinton kama mgombea ambaye yuko mbele katika njia ya kuweza kupata kuteuliwa na chama chake kwa ajili ya uchaguzi wa hapo Novemba 8 mwaka huu katika azma yake ya kuwa rais wa kwanza mwanamke nchini marekani.
Vituo mbali mbali vya televisheni vimeyaita matokeo hayo kwa Clinton mara tu baada ya kukamilishwa kwa upigaji kura, na kudokeza kwamba ni ushindi mkubwa. Matokeo ya awali yanaonesha akiwa ameshinda kwa kiwango kikubwa katika maeneo mengi.
Ushindi wa waziri huyo wa zamani wa mambo ya kigeni umeonesha nguvu zake miongoni mwa wapigakura wenye asili ya Afrika, ikiwa ni sehemu muhimu ya chama cha Democratic ambao wanafanya zaidi ya nusu ya wapiga kura wa awamu hii ya mchujo katika jimbo la South Carolina.
Matokeo mazuri ya tatu
Matokeo hayo ni ya tatu kwa Clinton katika majimbo manne ya mwanzo kugombaniwa na wagombea wa chama cha Democratic, na yamezusha maswali zaidi juu ya iwapo Sanders , seneta msoshalist wa chama cha Democratic kutoka jimboni Vermont, ataweza kupanua uungwaji wake mkono kupindulia ngome yake ya wazungu ambao ni waliberali.
"Leo mmetuma ujumbe," Clinton ameliambia kundi la waungaji wake mkono wakishangiria mjini Columbia baada ya matokeo kutangazwa. "Nchini Marekani , wakati tukisimama pamoja, hakuna kikwazo kikubwa ambacho hatutaweza kukivunja."
Sanders amekiri kushindwa mapema usiku huo wa Jumamosi.
"Lazima niwe muwazi katika jambo moja leo. Kampeni hii ndio kwanza inaanza. Tumeshinda ushindi muhimu New Hampshire. Ameshinda bila ubishi South Carolina. Sasa ni wakati wa "Jumanne kuu," Sanders amesema katika taarifa.
Mpambano unazidi kupanuka
Mbio za chama cha Democratic sasa zinakuwa mpambano mpana wa kitaifa. Majimbo 11, ikiwa ni pamoja na sita upande wa kusini yakiwa na idadi kubwa ya jamii za wachache ambako maoni ya wapiga kura yanaonesha Clinton anaongoza kwa kiwango kikubwa, watapiga kura katika Jumanne kuu na majimbo manne zaidi yatapiga kura mwishoni mwa juma.
"Kesho kampeni hii inageuka ya kitaifa," Clinton amesema.
Kambi ya Clinton ilikuwa na matumaini ya ushindi mkubwa South Carolina, baada ya ushindi mwembamba katika jimbo la Iowa na Nevada na ushindi wa wazi wa Sanders katika jimbo la New Hampshire, utamuweka Clinton katika hali ya kutarajia ushindi mkubwa siku ya Jumanne, wakati kiasi ya wajumbe 875 watapiga kura zao, zaidi ya theluthi moja kati ya wajumbe hao watahitajika ili kushinda nafasi ya uteuzi.
Sanders, ambae ameutia nguvu upande wa Waliberali katika chama hicho na kuwavutia vijana kupiga kura kwa ujumbe wake wa kushambulia uwiano wa mapato na kukaripia biashara ya soko la hisa la Wall Street, anahitaji kushinda katika jimbo muhimu katika wiki chache zijazo ili kuweka matumaini yake hai.
Mwandishi : Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Yusra Buwayhid