Clinton aongoza katika kura za maoni
26 Oktoba 2016Wagombea wote wawili wamewatolea wito wafuasi wao wajitokeze kwa wingi na kupiga kura Jumanne, Novemba 8, ambayo ni siku ya uchaguzi wa urais, kwa viti vyote vya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi pamoja na viti vipatavyo 33 vya baraza la Seneti lenye jumla ya viti 100.
Akiwa katika jimbo la Florida, mgombea wa chama cha Democratic, Hillary Clinton, amewasisitiza raia kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi. "Usingependa kuamka asubuhi ya Novemba 9, na kujiuliza kama ulifanya kila uwezalo na kama kuna zaidi ungeliweza kufanya katika uchaguzi", aliwaeleza Clinton.
Bi Clinton alihutubia siku moja tu kati ya siku mbili alizokuwepo jimbo la Florida. Utabiri unaionyesha njia ya Clinton kuwa ni safi kuelekea ushindi bila ya kulitegemea jimbo hilo la Florida. Clinton pia hakuchelewa kumpiga kijemba mshindani wake Donald Trump.
"Unajua mnamo Januari 20, jambo la kwanza ambalo rais analifanya ni kula kiapo cha kulinda na kuitetea katiba ya nchi , na ninamashaka makubwa kuhusu Donald Trump sidhani kama anaelewa maana ya kiapo hicho," amesema Hillary Clinton.
Kampeni ya Clinton imezidi kupata nguvu hivi karibuni, kufuatia kuungwa mkono na aliyekuwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani mrepublican, Colin Powell, wakati wa utawala wa George W. Bush kutoka mwaka 2001 hadi 2005.
Matokeo ya kura za maoni ya kitaifa yaliyochapishwa kwenye tovuti ya RealClearPolitics tangu katikati ya mwezi Oktoba, yanamuonesha Clinton kuwa anaongoza kwa zaidi ya asilimia 5. Na, kwa mujibu wa matokea yaliyotolewa Jumamosi na Shirika la habari la Reuters likishirikiana na Ipsos, Clinton alikuwa na uwezekano wa kushinda uchaguzi wa asilimia 95, kama ungefanyika wiki iliyopita.
Trump: Sera za Clinton juu ya Syria zitaleta Vita Vikuu vya Tatu
Kwa upande wake, mgombea wa chama cha Republican, Donald Trump, pia alikuwa jimboni Florida akifanya kampeni. Trump lazima ashinde jimbo la Florida, ili aongeza uwezekano wa kutimiza kura maalum 270 za kushinda urais. Trump alihudhuria hafla tatu tafauti za kampeni akiwa jimbo la Florida.
Clinton alitoa wito wa kuwekwa marufuku ya ndege kuruka katika anga la Syria, ili kuwalinda raia wasiohusika na mapigano. Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wameonesha wasiwasi kuhusu mpango huo, ambao wamesema huenda ukaitumbukiza Marekani katika mgogoro wa moja kwa moja na ndege za kivita za Urusi. Trump hakuchelewa kuliponda pendekezo hilo la mpinzani wake.
"Tunatakiwa kuliangazia kundi la IS na sio Syria. Mtatumbukia katika vita vikuu vya tatu mkimsikiliza Hillary Clinton," amesema Donald Trump.
Upigaji kura wa mapema utaanza Jumatatu jimbo la Florida. Zimebaki siku chache tu, hadi raia watakapo piga kura ya kuamua katika jimbo hilo la tatu kwa ukubwa wa idadi ya watu. Florida ni jimbo maarufu kwa kutokuwa na msimamo wa kuegemea chama kimoja. Linatambulika kama miongoni mwa majimbo yanayoweza kuamua matokea ya mwisho ya uchaguzi.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/rtre/dw
Mhariri: Gakuba Daniel