1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton ana kazi ngumu kuwashawishi wapigakura

Mohammed Khelef27 Julai 2016

Licha ya Hillary Clinton kuteuliwa rasmi kuwa mgombea urais wa Marekani kupitia Democrat, ukweli ni kuwa mwanamke huyo wa kwanza kuwania wadhifa huo ana kazi kubwa ya kuwaunganisha wapigakura wa chama chake.

https://p.dw.com/p/1JWgu
Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Democrat, Hillary Clinton.
Mgombea urais wa Marekani kwa tiketi ya Democrat, Hillary Clinton.Picha: Reuters/L. Jackson

Nje na ndani ya ukumbi wa mikutano mjini Philadelphia, wapinzani wa Clinton na waungaji mkono wa aliyekuwa mshindani wake, Bernie Sanders, wameweka wazi msimamo wao - kwamba upinzani wao kwa Donald Trump wa Republican ni kama ule walionao kwa Hillary Clinton. Hiyo ni hata baada ya Sanders mwenyewe kuwataka waache tafauti zao na kumuunga mkono Bi Clinton.

Usiku mzima wa jana uligeuzwa kuwa usiku wa harakati na maandamano. Maelfu ya wanaharakati wanaoupinga mfumo wa kitajiri na kitabaka nchini Marekani waliungana kuupinga uteuzi wa Bi Clinton.

Mmoja wao, Paula Olivares kutoka jimbo la Georgia, aliwaambia waandishi wa habari kuwa Mkutano Mkuu wa Democrat haukutenda haki. "Ninawakilisha hisia za mamilioni ya watu kote duniani ambao wamenichangia pesa kuja hapa kupigania demokrasia na kupambana dhidi ya ufisadi, wizi kwenye uchaguzi na ukandamizaji wa haki za mpigakura, ambao ndio unaoendelea sasa ndani ya Marekani ndani ya mwaka 2016."

Obama aitilia mashaka Urusi

Bi Clinton hakabiliwi na upinzani wa ndani ya chama chake tu. Kuna wasiwasi unaooneshwa wazi na Ikulu ya Marekani kuwa Urusi inajihusisha na siasa za ndani za uchaguzi huo, hasa baada ya tuhuma za kuchapishwa kwa barua-pepe za viongozi wa chama cha Democrat, ambazo zilionesha njama za uongozi huo dhidi ya kampeni za Sanders.

Aliyekuwa mwania tiketi ya Democrat kugombea urais wa Marekani, Bernie Sanders.
Aliyekuwa mwania tiketi ya Democrat kugombea urais wa Marekani, Bernie Sanders.Picha: Getty Images/AFP/N. Kamm

Akizungumza na kituo cha televisheni cha NBC, Rais Barack Obama, amekataa kuondoa uwezekano wa uingiliaji kati wa Urusi. Licha ya kuzungumzia moja kwa moja kuhusu udukuzi huo, lakini alisema anajuwa kuwa Trump amekuwa akiuzungumza vyema uongozi wa Urusi.

"Tunachojuwa ni kuwa Warusi wanafanya udukuzi kwenye mifumo yetu. Sio mifumo ya serikali pekee, bali hata ya watu binafsi." Alisema Obama.

Mara kadhaa, Trump amekuwa akisema waziwazi kwamba anauhusudu uongozi wa Rais Vladimir Putin wa Urusi, jambo ambalo linazua mashaka kuwa huenda Ikulu ya Kremlin inashiriki kumuwezesha bilionea huyo kuingia Ikulu ya White House.

Hata hivyo, muda mfupi uliopita, Kremlin imetoa taarifa ya kukanusha tuhuma hizo. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, amesema muda wote serikali ya Urusi imekuwa ikijiepusha na vitendo au maneno yanayoweza kutafsirika kuwa na athari ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja kwenye mchakato wa uchaguzi wa Marekani.

Mnamo mwezi Disemba, Rais Putin alinukuliwa akimsifia Trump kuwa ni "mtu madhubuti na mwenye kipaji cha hali ya juu."

Mwandishi: Mohammed Khelef/AP/AFP
Mhariri: Saumu Yussuf