Clinton akutana na wahanga wa ubakaji mashariki ya Goma
11 Agosti 2009Hillary Clinton alipowasili Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo kituo chake cha nne katika ziara yake ya nchi saba barani Afrika alisema:
"Leo niko hapa kuonyesha mshikamano wa Marekani na watu wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Tuna imani na matumaini na uwezo wenu na tunataka kuwa washirika wenu."
Leo Clinton akifuatana na maafisa wa ngazi ya juu amekwenda mji wa mashariki Goma ulio karibu na eneo ambako majeshi ya Kongo na Rwanda yalianzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa Kihutu katika mwezi wa Januari.
Katika eneo hilo lililoteketezwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe Clinton binafsi atazungumza na wahanga wa ubakaji. Hillary Clinton, mwanadiplomasia wa kike mashuhuri kabisa katika historia ya Marekani, hiyo jana alikutana na wanafunzi katika mji mkuu Kinshasa na alisema kuwa ubakaji ni miongoni mwa dhambi kubwa kabisa zinazofanywa na binadamu.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa tangu mwaka 1996,hadi wanawake 200,000 wamebakwa katika mashariki ya Kongo na vitendo hivyo vya unyama, vimezidi kuongezeka tangu majeshi kuanzisha operesheni zake katika eneo hilo. Umoja wa Mataifa unasema wote-wanamgambo na wanajeshi, wanahusika na uhalifu huo.
Clinton,alipozungumza na Radio Okapi alisema kuwa ubakaji na matumizi ya nguvu dhidi ya wanawake ni vitendo vinavyotumiwa kutisha na kudhalilisha umma. Amesema, ukatili wa aina hiyo ulishuhudiwa mwishoni mwa karne ya 20 na unashuhudiwa tena karne hii. Katika mahojiano mengine na kituo cha televisheni RagaTV, Clinton alisema, watu waliofanya vitendo vya ubakaji au ukatili wa ngono sio tu waone aibu bali wanapaswa pia kukamatwa na kufikishwa mahakani na kuadhibiwa ili liwe somo linalotuma ujumbe mkali kuwa vitendo kama hivyo havitovumiliwa.
Baadae leo hii, Hillary Clinton anakutana na Rais wa Kongo Joseph Kabila na amesema atamshinikiza Kabila kuimarisha hatua za kukomesha uhalifu na kuleta amani katika kanda hiyo. Wakati huo huo,Clinton amemsifu Rais Kabila kwa jitahada zake za kutafuta suluhisho la amani pamoja na viongozi wa nchi za jirani Rwanda na Uganda.Haki za wanawake ni mada iliyopewa kipaumbele wakati wa ziara yake ya nchi saba barani Afrika. Leo hii Clinton anarejea Kinshasa kabla ya kuelekea Nigeria.
Mwandishi: P.Martin / AFPE
Mhariri: M. Abdul-Rahman