Clinton aitaka Afrika Kusini kuishawishi Zimbabwe
7 Agosti 2009Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton ameitaka Afrika Kusini kushinikiza kuwepo kwa mageuzi ya kisiasa na uchumi katika nchi jirani ya Zimbabwe. Kauli hiyo ameitoa katika kituo chake cha pili cha ziara yake ya mataifa saba ya Afrika.
Akiwa nchini Afrika Kusini, hii leo Bibi Clinton anatarajia kukutana na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Afrika Kusini, ambapo watajadili mpango wa kumshinikiza Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe ili kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa baina yake na aliyekuwa kiongozi wa upinzani, Morgan Tsvangirai, ambaye kwa sasa ndiye Waziri Mkuu wa nchi hiyo katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Bibi Clinton amesema kuwa anatoa wito kwa Afrika Kusini kuwasaidia wananchi wa Zimbabwe wanaoteseka. Rais Mugabe, anayeiongoza nchi hiyo tangu ipate uhuru wake, amekuwa akikosolewa na nchi za Magharibi.
Baada ya mazungumzo hayo kwenye mji mkuu wa Afrika Kusini, Pretoria, Bibi Clinton atakutana na Rais wa zamani wa nchi hiyo, Nelson Mandela mjini Johannesburg. Aidha, Waziri huyo wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani atatembelea zahanati inayowaangalia waathirika wa virusi vya Ukimwi na hapo kesho Jumamosi ataeleka Durban kwa mazungumzo na Rais Jacob Zuma wa nchi hiyo na baadaye Cape Town ambako atashiriki katika shughuli za ustawi wa jamii.
Bibi Clinton amewasili nchini Afrika Kusini akitokea Kenya, ambako jana alifanya mazungumzo na Rais wa Serikali ya Mpito ya Somalia, Sheikh Sharif Ahmed. Katika mazungumzo yao, Bibi Clinton aliahidi msaada wa kifedha na vifaa vya kijeshi kutoka Marekani kwa ajili ya kuisaidia Somalia kupambana na wapiganaji wa Kiislamu. Bibi Clinton alisema:
'' Marekani inachukulia kwa makini sana vitisho vinavyotolewa na Al-Shabaab kwa watu wa Somalia, lakini pia watu wa eneo hilo kama hapa Kenya. Taarifa tulizonazo ni kwamba Al-Shabaab halitumii tu wapiganaji wa kigeni na hela za kigeni, lakini pia mawazo ya kigeni katika mashambulio yake kwa watu wa Somalia.''
Aidha, aliionya Eritrea kwamba Marekani inaweza kuiadhibu, endapo itaendelea kuwaunga mkono wapiganaji wa Al-Shabaab.
Bibi Clinton ataondoka Afrika Kusini kesho na kuendelea na ziara yake katika nchi za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Nigeria, Liberia na Cape Verde.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)
Mahariri: M.Abdul-Rahman