1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton afanya ziara ya muda mfupi Haiti

17 Januari 2010

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana hapo kesho kuzungumzia hali nchini Haiti.

https://p.dw.com/p/LXzI
Rais wa Haiti Rene Preval, akutana na Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton huko Port-au- Prince, HaitiPicha: AP

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton amekutana kwa mazungumzo na rais wa Haiti Rene Preval huko Port au -Prince. Clinton na Rais Preval walizungumzia suala la misaada kutoka Marekani, ambayo tayari imeanza kufika kisiwani Haiti, kufuatia maafa ya tetemeko la ardhi lililotokea wiki iliyopita. Mjini Washington, Rais Barack Obama alitangaza kuanzishwa kwa harambee ya kitaifa kuisadia Haiti itakayoongozwa na Marais wawili wa zamani wa Marekani, Bill Clinton na George Bush.

Haiti / Erdbeben / Port-au-Prince
Msichana mdogo asubiri matibabu, huko Petionville,katika mji wa Port-au-Prince, Haiti.Picha: AP

Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umezindua mpango wa kutafuta kiasi cha dola milioni 500 kuwasaidia wahanga wa tetemeho hilo la ardhi kisiwani Haiti. Mbali na misaada ya kiutu kama, maji chakula na makaazi afisa anayesimamia shughuli ya misaada ya Umoja wa Mataifa John Holmes ameitolea mwito Jumuiya ya Kimataifa kutafakari vipi watatoa msaada wa muda mrefu kwa watu wa Haiti. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon atawasili Haiti baadaye leo kujionea mwenyewe maafa ya tetemeko hilo la ardhi.

Bundesaußenminister Westerwelle / Japan
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle atangaza kuongezwa kwa msaada wa Ujerumani huko Haiti.Picha: AP

Hapa Ujerumani, Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Guido Westerwelle ametangaza kwamba raia mmoja wa Ujerumani aliuawa kufuatia tetemeko la ardhi huko Haiti. Westerwelle pia alisema kuna uwezekano idadi hii ikaongezeka, na kwamba Wajerumani 30 wametoweka baada ya tetemeko hilo la ardhi kukitingisha kisiwa hicho siku tano zilizopita. Westerwelle ambaye alikuwa ameandamana na Waziri wa maendeleo Dirk Niebel pia alitangaza Ujerumani itaongeza fedha za msaada kwa Haiti kutoka Euro Milioni 1.5 hadi Euro milioni 7.5. Timu ya madaktari wa Shirika la Msalaba Mwekundu nchini Ujerumani iliondoka jana kuelekea Haiti, na inatarajiwa kuwasili baadaye leo.