1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Clinton aelezea sera za nje za serikali mpya ya Marekani.

Halima Nyanza14 Januari 2009

Waziri Mteule Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, ameweka wazi vipaumbele watakavyotoa katika sera ya Mambo ya Nje ya serikali yao, ikiwa ni pamoja na kuzingatia diplomasia kwanza.

https://p.dw.com/p/GY1p
Waziri mteule wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton.Picha: AP

Waziri Mteule wa Mambo ya Nje wa Marekani Hillary Clinton ametoa maelezo hayo mbele ya Kamati ya Mambo ya Nje, ya Baraza la Senet, itakayomuidhinisha kama Waziri wa Masuala hayo, siku ya Alhamisi, ambapo aliahidi diplomasia kupewa kipaumbele katika sera za kigeni kwenye serikali yao mpya, na kwamba nguvu za kijeshi zitachukuliwa kama kimbilio la mwisho.


Katika kikao hicho Bibi Clinton kiaina aliukosoa utawala wa Rais anayemaliza muda wake George W Bush, kutokana na kutegemea sana nguvu ya kijeshi.


Amesema yeye na Rais Mteule Barack Obama wanaamini kuwa sera ya nje nilazima ijikite kwenye mawazo yakinifu, ukweli na maadili, na siyo itikadi ngumu, hisia au upendeleo wa chuki.


Waziri mteule wa Mambo ya Nje wa Marekani ameahidi pia uimara katika serikali yao na kusema kuwa ni lazima twatumie kile kilichoitwa ''utawala imara'', kutokana na nyenzo walizo nazo kidiplomasia, uchumi, jeshi kisiasa kisheria na kitamaduni.


Akizungumzia kuhusiana na mzozo unaoendelea sasa, Waziri Mteule wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema yeye na Rais mteule wa nchi hiyo wanaelewa uamuzi wa Israel kutaka kujilinda dhidi ya mashambulio ya roketi yanayofanywa na wapiganaji wa Hamas.


Ambapo pia ameelezea wasiwasi wake juu ya madhara wanayopata raia katika eneo hilo la Mashariki ya kati.


Lakini amesema huwezi kujadiliana na Hamas mpaka pale watakapoacha ghasia, kuitambua Israel pamoja na kukubali kutii makubaliano yaliyopita.


Hillary Clinton amesema ataendeleza juhudi, zilizoachwa na Waziri wa Mambo ya Nje anayemaliza muda wake Condolleza Rice katika kutafuta amani kwenye eneo hilo na kwamba kamwe nchi yake haitaacha kushughulikia mpango wa amani mashariki ya kati.


Aidha amesema serikali ya Barack Obama, ambayo inaingia madarakani Januari 20 itajaribu kutatua upya suala la Iran kwa kutumia misingi ya kidiplomasia, lakini ameonya kuwa nguvu zaidi zinaweza kutumia kuzuia nchi yake kurutubisha nyuklia.


Hillary Clinton ambaye uteuzi wake Kama Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, unatarajiwa kuidhinishwa rasmi na baraza la Seneta, muda tu baada ya kuapishwa kwa Rais Mteule Barack Obama, amesema katika sera zake za nje serikali yao mpya itaiongeza marafiki wapya, kuwa na washirika wengi na kupunguza orodha ya maadui wake.


Katika hatua nyingine, amesisitiza kuwa Marekani haiwezi kutatua matatizo peke yake na kwamba dunia pia haiwezi kuyatatua bila ya Marekani.


Aidha katika kikao hicho pia, Bibi Clinton alitahadharishwa na Seneta Richard Lugar wa Republican aliyetaka kuchukuliwa kwa hatua zaidi kuepusha mgongano wa kimaslahi kati ya kazi yake hiyo mpya ya uwaziri na taasisi ya mumewe, Rais wa zamani wa Marekani Bill Clinton, ambayo inajishughulisha kutoa misaada katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, umasikini na mapambani ya ukimwi, ambayo inapokea zaidi ya dila milioni 131 kutoka serikali za kigeni, ikiwemo Saud Arabia, Kuwait na Norway.