Chombo cha anga za juu Perseverence cha NASA chaelekea Mars
Chombo kipya cha anga za juu kwa jina Perseverence kimeanza safari kuelekea sayari ya Mars kufanya utafiti. Chombo hicho cha tano kurushwa na NASA kuelekea Mars ndicho kikubwa na kizito zaidi.
Kila kitu kiko tayari
Mnamo mwanzo wa Julai, wahandisi wa NASA walikiweka chombo Perseverence cha kuelekea Mars kwenye roketi ya Atlas V. Roketi hiyo itarushwa Julai 30 eneo la Cape Canaveral, Florida. Chombo hicho kinatarajiwa kuwasili Mars Februari 2021.
Maonyesho ya chombo hicho
Hivi ndivyo chombo hicho kilivyoonekana kilipoonyeshwa kwa umma mwaka uliopita. Kitasaidia chombo kilichokitangulia cha NASA kwa jina Curiosity katika sayari Mars. Curiosity ndicho kilikuwa chombo cha kisasa zaidi hadi Perseverence kilipotengenezwa. Perseverence kina uzito wa tani moja zaidi ule wa Curiosity. Kina urefu wa mita tatu, ambayo ni sentimita 10 zaidi ya urefu wa Curiosity.
Kazi ya ziada
Chombo Perseverence kinaweza kuwekewa vifaa zaidi vya utafiti kuliko 'mtangulizi' wake. Mikono yake, kamera na ala nyingine zina nguvu zaidi. Chombo hicho kinaweza kukusanya sampuli katika sayari ya Mars. Kimewekewa kamera 23 na ala nyingine. Dhamira yake moja ni kubaini uwezekano wa kupata hewa safi yaani oksigeni kwenye mawe ya Mars. Lakini hebu tazama, ni nini hicho kimesimama karibu nacho?
'Drone' ndogo
Naam! Chombo Perseverence kina helikopta aina ya drone. Hilo halijawahi kufanyika kwa vyombo vya anga za juu vinapoelekea kutafiti sayari nyingine. Matumizi ya helikopta ni jambo jipya kabisa. Itakuwa mara ya kwanza watafiti wataijaribu na kuitumia kukusanya data katika angahewa ambayo ni tofauti na ya dunia na pia katika mvuto wa sayari yaani 'gravity' ambao ni theluthi moja ya wa dunia.
Jitu la roboti
Chombo Curiosity ndicho kilikuwa kikubwa na cha kisasa zadi kupelekwa Mars. Kiliwasili Agosti 16, 2012 na tayari kimefanya safari ya kilomita 21. Si chombo tu kinachosafiri. Jina lake rasmi ni Maabara ya Kisayansi ya Mars, na kwa hakika ni maabara kamili inayosafiri.
Kina vitu gani?
Kwa mfano, kina vifaa vya kupima kemikali zitakazogunduliwa Mars, kina kituo kizima cha utabiri wa hali ya hewa kinachoweza kupima viwango vya joto, presha angani, mionzi, unyevu, kasi ya upepo lakini ya muhimu zaidi ni kwamba kina maabara ya kemia kinachoweza kufanya tathmini ya sampuli za vitu vilivyomo humo kando na kutafuta alama ya ikiwa kuna viumbe vipya.
Si kazi ya juu juu tu
Kinadharia, chombo Curiosity kimeonyesha kuna uwezekano wa kuwa na uhai katika sayari Mars. Lakini bado hakijabaini kiumbe chochote hai. Chombo hicho kina kifaa madhubuti cha kuchimba. Hapa kinakusanya sampuli kwenye volkano.
Shughuli katika maabara
Michanga ya Mars hushughulikiwa na ala nyingi. Kwanza huchujwa, kuchungwa na kugawanywa katika mafungu tofauti kulingana na saizi zao. Kisha inafanyiwa vipimo tofauti kutumia mashine mbalimbali kwenye maabara.
Chombo kidogo cha awali
Vyombo vilivyokitangulia Curiosity kupelekwa Mars, vilikuwa vidogo. Mnamo Julai 4, 1997, chombo kidogo kwa jina Sojouner, kiliweka alama za magurudumu yake kwenye sayari Mars. Hiyo ilikuwa mara ya kwanza roboti linalosafiri kuachwa kutegema vifaa vilivyowekewa, ikiwa ni pamoja na chombo cha X-ray pamoja na kamera kufanya vipimo na tathmini.
Ulinganishaji wa ukubwa
Hadi sasa kuna vizazi vitatu vya vyombo vya anga za juu kuitafiti Mars. Sojourner ilikuwa na uzito wa kilo 10.6. Ukubwa wake ulikaribia wa kijigari kidogo. Kilikwenda kwa kasi ya sentimita moja kwa sekunde. Chombo kwa jina Opportunity kilikuwa na uzito wa kilo 185. Nacho Curiosity kilikuwa na uzito wa kilo 900. Vyombo hivyo vikubwa vinasafiri kwa kasi ya sentimita 4 au tano kila sekunde.
Takriban miezi minne ya utafiti
Katika kipindi chake, chombo Sojourner kilisafiri jumla ya mita 100 na kuwasilisha data pamoja na picha hadi Septemba 27, 1997. Picha hii ni miongoni mwa zile za mwisho kuwasilishwa na chombo hicho, siku tisa kabla ya masafa yake ya redio yaliyotumiwa kimawasiliano kukatika. Huenda chombo hicho Sojourner kiliharibika kwa sababu ya betri yake kushindwa kustahimili baridi nyakati za usiku.
Kuandaa njia kwa ajili ya teknolojia ya kesho
Bila ya data zilizokusanywa na Sojourner, huenda kusingekuwa na fikra ya kuunda vyombo vipya. Mwaka 2004, NASA ilipeleka maroboti mawili Spirit na Opportunity katika sayari Mars. Spirit ilidumu kwa miaka 6 na kusafiri jumla ya kilomita 7.7. Roboti hilo lilikwea milima na lilikusanya sampuli. Lakini roboti Opportunity lilipoteza mawasiliano mnamo Februari 13, 2019.
Ala kibao
Mnamo mwaka 2005, roboti Opportunity lilikuwa limesafiri umbali wa kilomita 42, na hadi leo limeendelea kusafiri kilomita nyingi kuliko chombo Curiosity. Linaweza kutumia mkono wake kuchunguza ardhi. Lina vifaa vitatu tofauti vya vipimo pamoja na kamera ya 3D. Mara ya mwisho ilikuwa ikifanya utafiti katika Bonde la Perseverance kabla ya kulemewa na kimbunga kutokana na mchanga.
Mazingira ya sayari nyekundu (Mars)
Picha hii ilipigwa na kamera ya roboti Curiosity. Chombo cha kisasa zaidi kinaweza kudumu katika sayari Mars kwa muda mrefu zaidi, ikiwezekana miaka isiyopungua mitano. Muonekano wa ardhi ya Mars unaonekana kuwa wa kawaida. Je unafikiri tunaweza kujipeleka katika sayari hii ya kuvutia au tuache Mars kwa Maroboti tu?