1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chombo cha anga cha China chatua karibu na mwezi

Sylvia Mwehozi
3 Januari 2019

Chombo cha anga cha China kimefanikiwa kutua sehemu inayojulikana kuwa ya giza Mwezini na kulifanya taifa hilo kukaribia kuwa lenye nguvu katika masuala ya anga.

https://p.dw.com/p/3B05z
China Mondsonde "Chang'e-4"
Picha: picture-alliance/Xinhua

Mataifa matatu, Marekani, uliokuwa umoja wa Kisovieti na sasa China ndizo ambazo zimetuma vyombo vyake karibu na sehemu ya mwezi inayotazamana na dunia. Lakini kutua kwa chombo cha China kinachoitwa Chang'e 4, kunaelezwa kuwa wa historia katika sehemu hiyo ya mbali, na kuzidisha shauku yake ya kushindana na Marekani, Urusi na Ulaya katika masuala ya anga.

Kutua kwa chombo hicho, kumetangazwa na vyombo vya habari vya China. Mwaka 2013 chombo kingine cha awali cha Chang'e 3 kilifanikiwa kutua kwa mara ya kwanza katika mwezi tangu chombo kingine cha Luna 24 kutoka uliokuwa Umoja wa Kisovieti kilipotua mwaka 1976. Marekani ni nchi pekee ambayo imefanikiwa kutuma mtu katika mwezi, ingawa China inafikiria kutuma ujumbe wa watu pia.

Rückseite des Mondes von der Mondsonde Chang'e-4
Picha iliyotumwa na chombo hiko baada ya kutua sehemu ya mbali ya mwezi Picha: picture-alliance/Xinhua News Agency

Kwa hivi sasa inafikiria kutuma chombo kingine cha Chang'e 5 ili kikafanye uchunguzi katika Mwezi hapo mwakani na kitarudi na sampuli duniani, kitu ambacho hakijawahi kufanyika tangu mwaka 1976. Sehemu hiyo ya mbali ya mwezi huwa si ya giza kila wakati lakini wakati mwingine inafahamika hivyo kwasababu inakuwa mbali sana na dunia na kiasi haijulikani. Ina muundo wa tofauti na ule wa sehemu ya karibu, ambako vyombo vingine vya awali vilitua.

Hadi sasa changamoto iliyopo kutoka sehemu hiyo ya mbali ya mwezi ni mawasiliano na dunia. China ilianzisha mtambo wa satelaiti mwezi Mei ili chombo cha Chang'e 4 kiweze kutuma taarifa.

mwandishi: Sylvia Mwehozi/ap

Mhariri: Sekione Kitojo