1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CHITUNGWIZA :Mugabe atetea kutoialika Ulaya kwenye uchaguzi

13 Machi 2005
https://p.dw.com/p/CFXc

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe hapo jana ametetea uamuzi wake wa kutozialika nchi za Umoja wa Ulaya kuangalia uchaguzi wa bunge wa mwezi huu kwa kusema kwamba Ulaya inapaswa kutoingilia kati masuala ya ndani ya Zimbabwe.

Mugabe aliwaambia wafuasi wake katika ngome kuu ya upinzani ya Chitungwiza kwamba wamezialika nchi nyingi lakini sio wazungu ......kama akina Blair (Waziri Mkuu wa Uingereza) na wengine wa Ulaya.

Amekaririwa akisema hawapaswi kuingilia kati, wanapaswa kubakia katika nchi zao ambako wanatawala na sio hapo.

Russia ni nchi pekee ya Ulaya kati ya nchi 32 zilizoalikwa kufuatilia uchaguzi huo wa bunge uliopangwa kufanyika tarehe 31 mwezi wa Machi.

Mugabe amewaambia wafuasi wake hao litakuwa telekezo kwake yeye na kwa chama chake iwapo wataupigia kura upinzani.

Zimbawe iligoma kuziruhusu nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani kuangalia uchaguzi wa Rais wa mwaka 2002 ambao uliingia dosari kutokana na madai ya matumizi ya nguvu, vitisho na ulaghai wa kura.