1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yataka Marekani, K. Kaskazini ziache hatua za kijeshi

8 Machi 2017

Wakati ushindani kati ya majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini na mazoezi ya kijeshi ya Korea Kusini na Marekani ukiendelea, China imezitaka pande zote mbili kusitisha hatua zao zinazotishia usalama.

https://p.dw.com/p/2YonS
China Wang Yi
Picha: picture alliance/dpa/VCG

Pendekezo la China kwenye kile inachokiita "usitishwaji wa mara mbili" linalenga kuifanya Rasi ya Korea isiingie kwenye mzozo usioweza kutatuka tena kwa majadiliano, kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Kigeni wa China, Wang Yi.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Beijing hivi leo kandoni mwa mkutano mkuu wa chama tawala cha kikomunisti, Wang alisema ukweli ni kuwa Rasi ya Korea inashuhudia kuongezeka kwa hali ya wasiwasi kwa sababu Korea Kaskazini inajaribu makombora yake ya masafa marefu, huku Marekani na Korea Kusini zikiendelea na mazoezi ya pamoja ya kijeshi, na endapo hali itaendelea hivi, kitisho cha mapigano kipo wazi.

"Kuukwamuwa mkwamo huu, China inapendekeza kwamba katika hatua ya awali Korea Kusini isitishe shughuli zake za kinyuklia na makombora, nazo Marekani na Korea Kusini zisitishe mazoezi yao ya kijeshi. Hili tu ndilo linaloweza kututoa kwenye njia panda na kuzipeleka pande hizi mbili kwenye meza ya mazungumzo", alisema Wang.

Nordkorea Raketentest bei Hwasong
Korea Kaskazini ilifanya majaribio ya makombora kujibu hatua za Marekani na Korea Kusini kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi kwenye Rasi ya Korea.Picha: Reuters/KCNA

Korea Kaskazini ilifanya majaribio ya makombora yake siku ya Jumatatu, ikijibu hatua za Marekani na Korea Kusini kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi kwenye eneo hilo. Korea Kaskazini ilirusha makombora manne kuelekea pwani ya kaskazini magharibi mwa Japan, yakiwa majaribio ya karibuni zaidi yanayokaidi vikwazo vya Umoja wa Mataifa.

Lakini sasa China, ambayo kawaida huwa inaikingia kifua Korea Kaskazini, inaonesha kutishwa na kuchoshwa na uhasama huu unaohatarisha maslahi yake kwenye eneo hilo. Licha ya kujitenga na majaribio haya ya makombora, Rais Donald Trump wa Marekani anaitaka China ichukuwe hatua zaidi za kuizuia Korea Kaskazini kuendelea na kile anachokiita "uchokozi", mada ambayo China inasema si sahihi.

"Suala la nyuklia kwenye Rasi ya Korea linazihusu zaidi Korea Kaskazini na Marekani. China na jirani wa karibu sana na mwenye uhusiano mkubwa na Rasi yenyewe. Kwa hivyo, lazima tunakuwa sehemu muhimu ya utatuzi wa suala hili la nyuklia. China inadhamiria kwa dhati kulifanya eneo hili lisiwe na silaha za nyuklia, kudumisha utulivu na kutatua mzozo huu kwa amani", alisema Wang.

Katika mkutano uliondaliwa na Umoja wa Mataifa juu ya kuachana na silaha kali mjini Geneva hapo jana, balozi wa Korea Kaskazini kwenye Umoja huo, Ju Yong Choi, alisema mazoezi ya kila mwaka ya kijeshi yanayofanywa na Marekani kwenye eneo lao, ndicho chanzo kikuu cha mzozo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman