China yazidisha luteka za kijeshi kwa Taiwan
15 Agosti 2022Wabuge hao wamekutana na Rais Tsai Ing-wen, hatua ambayo serikali ya Beijing inaiita ni kuingiliwa uhuru wake wa kimipaka.
Wabunge hao watano wa Marekani, wakiongozwa na Seneta Ed Markey, waliwasili mjini Taipei jana Jumapili katika ziara ya kushtukiza, ukiwa ni ujumbe wa ngazi ya juu wa pili kuwasili katika eneo hilo, baada ya ule wa Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi, uliofika katika eneo hilo mapema Agosti na kusababisha vitisho kadhaa vya kivita.
Kikosi cha jeshi la China ambacho kina dhamana ya kudhibiti hali ya usalama kwenye eneo linalotazamana na Taiwan, kiitwacho-People's Liberation Army's Eastern Theatre Command- kimesema kimeandaa doria za utayarifu wa mapambano katika eneo la bahari na anga karibu ya Taiwan.
China imesema ziara ya wabunge wa Marekani Taiwan inakiuka uhuru wake.
Katika taarifa nyingine tofauti Wizara ya Ulinzi ya China imesema kwamba safari ya wabunge hao inakiuka uhuru wa China na kuweka wazi nia ya dhati ya Marekani kama mharibifu wa amani na utulivu kwenye eneo la Ujia wa Bahari wa Taiwan. Taarifa hiyo iliendelea kusema kikosi hicho cha China kitaendelea kufanya mafunzo na kujiandaa na vita, kulinda uhuru wa mipaka yake na kuapa kusambaratisha kile lilichokiita uhuru wa kujitenga kwa Taiwan na uingiliaji wa kigeno.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Taiwan Su Teseng-chang amesema vitisho vya China havitawazuia kuwa na marafiki wa mataifa ya kigeni. Kauli kama hiyo imetolewa na mbunge kutoka chama cha Demkrasia cha Taiwan, Lo Chih-cheng."Ujumbe huu ni muhimu sana katika kipindi hiki na pia ni muhimu zaidi kwa sababu lengo la mazoezi ya kijeshi ya China ni kuwazuia wawakilishi wengine wa Marekani kuzuru Taiwan. Na ziara hii kwa mara nyingine tena inaonesha China haiwezi kuamuru au kuelekeza mataifa mengine, wanasiasa kutoitembelea Taiwan. Vilevile inaonesha na kupeleka ujumbe muhimu kwamba watu wa Marekani wapo pamoja na Taiwan."
Soma zaidi:Taiwan yaanza mazoezi ya ufyatuaji mizinga
Ziara ya mapema Agosti ya Spika wa Bunge la Marekani iliikasirisha China, ambayo kwa mara ya kwanza ilijibu kwa kurusha makombora katika maeneo ya karibu na Tipei kwa mara ya kwanza. Lakini kundi hili la sasa wa wabunge wa Marekani nalo leo hii linatarajiwa kukutana na Rais Tsai. Marekani haina mahusiano rasmi ya kidemokrasia na kiswa cha Taiwan, lakini kimsingi inawajibu ya kutoa usaidizi katika jitihada ya kujilinda chenyewe.
Chanzo: RTR