China yaondoa vizuizi vyote vya UVIKO-19 kwa wasafiri
8 Januari 2023China hata hivyo inachukua hatua hatua hiyo wakati ikipambana na ongezeko la visa vya UVIKO. Watu wa kwanza kuwasili China bara walielezea ahueni kwa kutolazimika kuingia karantini kitu ambacho kilifanywa mara zote wakati China ilipotangaza sera kali ya kupambana na ugonjwa huo.
Na katika kisiwa cha Hong Hong, ambako mpaka na China bara umefunguliwa baada ya miaka kadhaa ya kufungwa, zaidi ya watu 400,000 wanatarajiwa kuingia China katika wiki nane zijazo.
Beijing mwezi uliopita ilianza kuondoa mkakati wake imara wa kupambana na UVIKO ambao ulihitaji kuwepo karantini za lazima na kuwafungia watu kusafiri. Sera hiyo ilikuwa na athari kubwa kwa nchi hiyo ya pili kubwa kiuchumi uliwenguni na kuzusha hasira ya umma ambayo ilipelekea maandamano ya kitaifa kabla ya kulegezwa.
"Nadhani ni vizuri kwamba ile sera imebadilishwa sasa. ni jambo la kiutu sana," aliliambia AFP. "Ni hatua muhimu, nadhani. UVIKO imekuwa ni ugonjwa wa kawaida duniani kwa sasa, na baada ya vihunzi vya hapa na pale, nadhani mambo yatakuwa mazuri tu," aliongeza.
Watu wa China walianza kupanga safari za nje baada ya mwezi uliopita serikali ya Beijing kutangaza kwamba itaondoa karantini kwa wasafiri.
Lakini, kwa upande mwingine hatua hii inayoashiria kuongeza idadi ya wasafiri imeyasukuma mataifa mengine kuanzisha vizuizi vya udhibiti wa mlipuko wa janga hilo kama upimaji wa lazima wa UVIKO-19 kwa wasafiri wanaotoka nchini China.
Hata hivyo China imekosoa hatua hizo za kimataifa ikiziita zisizokubalika, licha ya kuwazuia kwa kiasi kikubwa watalii kutoka mataifa ya kigeni pamoja na wanafunzi kusafiri.
Maambukizi yanaweza kuongezeka katika sherehe za mwaka mpya wa China.
Mlipuko wa UVIKO-19 nchini China unatabiriwa kuongezeka zaidi hasa katika sherehe za mwaka mpya wa China mwezi huu, ambapo mamilioni wanatarajiwa kusafiri kuzoka kwenye miji iliyoathiriwa pakubwa na maambukizi ya virusi vya UVIKO-19, wanaowenda kuwatembelea jamaa zao kwenye maeneo mengine, na hasa wazee ambao wako hatarini zaidi kuambukizwa.
Kwenye uwanja wa Beijing mapema leo, hakukuwa na vizuizi ambavyo viliwekwa awali katika eneo la kuwapokea wasafiri wa ndani.
Mwanamke mmoja, aliyekuwa akimsubiri mgeni wake, alisema watakachokifanya kwanza ni kupata mlo baada ya kumpokea. "Ni furaha kubwa, hatujaonana kwa muda mrefu sana," Wu, 20, aliliambia AFP.
Kwenye uwanja wa ndege wa Shanghai, mwanaume mmoja aliyejitaja jina moja la Yang, aliyekuwa akitokea Marekani alisema hakuwa anajua kwamba vizuizi hivyo vimeondolewa. "Sikujua", aliliambia AFP. "Ninajiona kama mwenye bahati sana, na hasa kwa sababu sitakiwi kukaa karantini, na hakuna makaratasi ya kujaza, yaani naondoka tu, kama huko nyuma... nina furaha sana."
Na katika jiji la Hong Kong, wageni walionekana kumiminika kutoka maeneo mbalimbali kupitia mipakani baada ya vizuizi kulegezwa.
Na katika kituo cha ukaguzi cha Lok Ma Chau karibu na Shenzhen, mwanafunzi aliyetokea China Bara, alyejitaja jina moja Zeng aliiambia AFP kwamba alikuwa na furaha mno kusafiri bila ya kuwepo na kizuizi chochote. "Nina furaha kwa kuwa sitakiwi kukaa karantini-- hakuna mtu alikuwa anapenda," Zeng aliiambia AFP.