1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaionya Marekani kuhusu usalama wa Asia

21 Mei 2014

Rais Xi Jinping wa China ameionya Marekani na nchi nyengine kuhusiana na suala la usalama wa Asia na kutowa wito wa kuundwa kwa ushirikiano mpya wa usalama barani Asia utakaojumuisha Urusi na Iran na kutoingiza Marekani.

https://p.dw.com/p/1C3kG
Baadhi ya viongozi wa Asia waliohudhuria mkutano wa CICA Shanghai.( 21.05.2014)
Baadhi ya viongozi wa Asia waliohudhuria mkutano wa CICA Shanghai.( 21.05.2014)Picha: Reuters

Rais Xi Jinping wa China ameionya Marekani na nchi nyengine kuhusiana na suala la usalama wa Asia onyo lake hilo linafuatia wito wake alioutowa jana wa kanzisha muundo mpya wa ushirikiano wa usalama barani Asia chini ya msingi wa kundi la kanda utakaoijumuisha Urusi na Iran na kutoingiza Marekani.

Akizungumza katika mkutano wa kanda ya Asia kuhusu usalama mjini Shanghai Rais Jinping wa China ameionya Marekani katika onyo lisilo wazi kwa kusema kwamba mataifa hayapaswi kuunda muungano wa kijeshi barani Asia wakati China ikifarakana na majirani zake.Amesema China itatumia njia za amani kutatuwa mizozo ya maeneo.

China imekuwa ikipingana na sera ya kigeni ya Marekani kwa Asia na pia imekuwa ikiziudhi Vietnam na washirika wawili wa Marekani,Japani na Ufilipino katika kile nchi hizo ilichokiita kuwa hatua zake za uchokozi katika mizozo tafauti ya maeneo ya bahari.

Rais Jinping bila ya kuzitaja nchi kwa majina amesema kuimarisha au kujenga muungano wa kijeshi kwa kuilenga nchi fulani hakuleti tija katika kudumisha usalama wa pamoja.

Onyo lake hilo la leo linafuatia wito wake alioutowa hapo jana wa kutaka kuanzishwa kwa muundo mpya ya ushirikiano wa usalama barani Asia utakozijumuisha Urusi na Iran bila ya Marekani.

Ushirikiano wa kijeshi na Urusi

Rais Vladimir Putin wa Urusi ambaye yuko ziarani nchini China pia alihudhuria mkutano huo wa Mashirikiano na Kujenga Imani barani Asia unaoujulikana kwa kifupi CICA na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya majeshi ya nchi hizo mbili na wizara zao za ulinzi.Amesema ushirikiano huo ni muhimu sana katika kudumisha amani katika kanda na dunia.

Rais Vladimir Putin wa Urusi (kushoto) na Rais Xi Jinping(kulia) mjini Shanghai.( 21.05.2014)
Rais Vladimir Putin wa Urusi (kushoto) na Rais Xi Jinping(kulia) mjini Shanghai.( 21.05.2014)Picha: Reuters

Hapo jana Rais Putin wa Urusi na mwenzake wa China walizinduwa mazoezi ya majeshi ya majini nje ya mwambao wa Shanghai na leo wamefikia makubaliano yaliokuwa yakisubiriwa kwa muda mrefu kwa Urusi kuipatia gesi ya asili China ambayo ina mahitaji makubwa ya nishati.

Viongozi kadhaa wa Asia ya Kati walihudhuria mkutano wa CICA ambapo nchi wanachama wake 24 ni pamoja na Korea, Thailand na Uturuki.Kabla ya kuanza kwa mkutano huo Rais Jinping wa China alipeana mikono na viongozi wengne wa nchi wanaohudhuria mkutano huo akiwemo Rais Vladimir Putin wa Urusi, Hassan Rouhani wa Iran na Hamid Karzai wa Afghanistan.

Mfarakano wa China na Vietnam

Matangazo ya moja kwa moja ya televisheni ya taifa ya China yaliruka sehemu iliyoonyesha Makamo wa Rais wa Vietnam Nguyen Thi Doan akipeana mkono na Rais Xi Jinping.

Maandamano dhidi ya China katika mji wa Chi Minh,Vietnam.
Maandamano dhidi ya China katika mji wa Chi Minh,Vietnam.Picha: Reuters

Uhusiano kati ya China na Vietnam umefikia katika hali mbaya sana kuwahi kushuhudiwa baada ya China kuweka rigi la utafiti wa kuchimba mafuta katika maeeno ya bahari yenye mzozo kwenye Bahari ya China Kusini mapema mwezi huu.

Hatua yao hiyo imezusha maandamano ya ghasia nchini Vietnam ambapo raia wanne wa China waliuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa na kupelekea China kuwahamisha maelfu ya raia wake kutoka Vietnam.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/AP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman