Taiwan: Blinken ailaumu China kwa luteka zake za kijeshi
5 Agosti 2022Wizara ya ulinzi ya Taiwan imesema jumla ya ndege 68 za kijeshi za China na meli 13 za jeshi la wanamaji ziliendesha luteka katika mlango wa bahari ya Taiwan na kwamba baadhi ya mazoezi hayo ya kijeshi kwa makusudi yalivuka eneo lisilo rasmi linalotenganisha pande mbili hizo. Wizara hiyo imeilaani China. Katika taarifa yake, imesema hatua ya vikosi vya kijeshi vya China ya kufanya luteka katika eneo hilo nyeti imevuruga hali ya utulivu iliyokuwepo na imekiuka sheria kwa kuingia katika eneo la bahari na anga ya Taiwan.
Watu wa kisiwa cha Liuqiu, kilichoko kilomita 13 kusini-magharibi mwa kisiwa kikuu cha Taiwan na mojawapo ya sehemu iliyo karibu zaidi na eneo lilikofanyika luteka za kijeshi China, leo Ijumaa wameonesha hisia tofauti kuhusu mazoezi hayo juu ya usalama wao.
Jeshi la China limesema katika taarifa yake kwamba limefanya mazoezi ya anga na baharini kaskazini, kusini magharibi na mashariki mwa Taiwan na linaendelea na luteka hizo ili kupima uwezo wa pamoja wa wanajeshi wake.China ilizindua mazoezi hayo makubwa zaidi ya kijeshi kuwahi kutokea katika bahari na anga karibu na Taiwan hpo jana Alhamisi siku moja baada ya ziara ya Nancy Pelosi katika kisiwa hicho.
Soma Zaidi:China yamuwekea vikwazo Pelosi
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imesema imemwekea vikwazo Spika wa Baraza la Wawakilishi la Marekani Nancy Pelosi na familia yake, hata hivyo vikwazo hivyo havijabainishwa. Wizara hiyo imesema ziara ya Pelosi ni uingiliaji mkubwa wa mambo ya ndani ya China. Wizara ya mambo ya nje ya China imesema Beijing pia inasitisha mazungumzo na Washington katika masuala kadhaa muhimu ikiwa ni pamoja na sera ya ulinzi, uratibu, ushirikiano wa kuwarejesha nyumbani wahamiaji haramu na usaidizi wa kisheria katika masuala ya jinai.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema China inajaribu kubadili utaratibu uliopo katika mlango wa bahari ya Taiwan kwa kufanya majaribio ya makombora na mazoezi ya kijeshi. Amesema ukweli ni kwamba ziara ya Pelosi ilikuwa ya amani na hivyo hakuna uhalali wa hatua hizi zilizopita kiasi. Blinken ameyasema hayo katika mkutano wa baraza la mawaziri wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini-Mashariki ya Asia (ASEAN) katika mji kuu wa Cambodia, Phnom Penh.
Angalia:
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, Hua Chunying, amesema China inaitaka Marekani kuacha mara moja kuboresha uhusiano na eneo la Taiwan, na kusimamisha mara moja kuiuzia Taiwan silaha. Amesema ikiwa kweli Marekani inawajibika, ingezuia ziara ya Pelosi ya uchokozi huko Taiwan!. Vilevile Marekani inapaswa kuondoa idadi yake kubwa ya ndege za kijeshi na meli za kivita katika eneo la Asia-Pasifiki.
Serikali ya Marekani ilitangaza hapo jana kuwa imeahirisha majaribio yalilyokuwa yamepangwa kwa muda mrefu ya makombora ya masafa marefu ili kuepusha mvutano unaozidi kuongezeka kati yake na China.
Vyanzo:DPA/RTRE