1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yafungua daraja refu zaidi duniani

Admin.WagnerD23 Oktoba 2018

China imefungua daraja refu zaidi duniani linalokatisha bahari kuunganisha bara ya China na eneo lenye utawala wa ndani la Hongkong katika kile kinachoonekana kuwa alama ya uhodari wa taifa hilo kwenye sekta ya uhandisi.

https://p.dw.com/p/36zfw
China Eröffnung Hongkong-Zhuhai-Macau-Brücke
Picha: picture-alliance/dpa/MAXPPP

Rais wa China Xi Jinping aliongoza sherehe za ufunguzi wa daraja hilo lenye urefu wa kilometa 55 linaloyaunganisha maeneo mawili ya Hong Kong na Macau.

Sherehe hizo za ufunguzi zilizopambwa kwa onesho la ufyatuaji fashifashi zilifanyika jana kwenye mji wa Zhuhai na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa miji ya Hongkong na Macau.

Ujenzi wa daraja hilo lililovunja rikodi umeigharimu China dola za kimarekani bilioni 20 na imechukia kiasi muongo mmoja kumaliza ujenzi wake, hali iliyoongeza gharama ikilinganishwa na makadirio ya hapo kabla.

Daraja hilo, ambalo limejengwa kuhimili matetemeko makubwa ya ardhi na vimbunga, linajumuisha njia ya urefu wa kilimota 30 iliyopita kwenye mlango wa Mto Pearl na linajumuisha pia visiwa viwili vidogo vya kujengwa na binadamu .

Ufunguzi wake utapunguza muda wa safari kutoka Hong Kong hadi bara ya China kwa hadi dakika 30 badala ya saa nne, jambo ambalo China inatumai itakuwa kiungo muhimu kwa ukuaji wa uchumi katika siku zijazo.

Kiungo muhimu kati ya bara ya China na Hong Kong

Eröffnung  Hongkong-Zhuhai-Macao-Brücke Xi Jingping
Picha: picture alliance/AP Photo/A. Wong

Daraja hilo jipya linakuwa kiungo rasmi kati ya bara ya China na Hongkong, eneo ambalo ni kitovu cha biashara barani asia, lililokabidhiwa kwa China kutoka uingereza mwaka 1997 kwa makubaliano ya kusalia na mifumo ya ndani ya sheria na uchumi kwa miaka 50 .

Ufunguzi wake unabeba mafanikio makubwa ya kisiasa ya utawala wa Rais Xi ambao mara kadhaa umepuuza miito ya kutaka mageuzi ya kisiasa ndani ya Hongkong hali inayoleta wasiwasi kuwa Beijing itaongeza ukandamizaji wa haki za raia kabla ya kufikia mwisho wa mpango uliopewa jina la 'Nchi moja mifumo miwili' hapo mwaka 2047.

Waungaji mkono wa daraja hilo wanaona ujenzi wake ni mafanikio muhimu kuelekea ukuaji zaidi wa uchumi na kupunguza muda wa safari lakini wakosoaji wake wanasema daraja hilo halitakuwa na mafao yoyote kwa uchumi, na lengo muhimu ni kuhakikisha Hong Kong inaunganishwa na bara ya China.

Kuna athari za mazingira?

Hangzhou Bay-Brücke
Picha: Getty Images/Guang Niu

Kumekuwa pia na wasiwasi kuhusu athari za mazingira zilizotokana na ujenzi wa daraja hilo.

Makundi ya kutetea uhifadhi wa mazingira yanasema mradi huo huenda umeathiri sana viumbe wa baharini, ikiwa ni pamoja na pomboo weupe wa China ambao ni miongoni mwa viiumbe vilivyo hatarini kutoweka.

Kulingana na Ofisi ya Fuko la Kuhifadhi Wanyamapori WWF tawi la Hongkong Idadi ya pomboo wanaoonekana katika bahari ya Hong Kong imepungua kutoka 148 hadi 47 katika miaka 10 iliyopita, na hakuna pomboo aliyeonekana karibu na daraja hilo.

Mwandishi: Rashid Chilumba

Mhariri: Iddi Ssessanga