1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China yaadhimisha miaka 70 ya ushindi dhidi ya Japan

3 Septemba 2015

China imeonyesha nguvu yake ya kijeshi katika kumbukumbu ya ushindi dhidi ya Japan katika vita vikuu vya pili vya dunia, tukio lililodhihirisha imani inayoongezeka ya utawala mjini Beijing katika vikosi vyake vya ulinzi.

https://p.dw.com/p/1GQR9
Rais wa China Xi Jinping akitoa hotuba katika uwanja wa Tianmen mjini Beijing.
Rais wa China Xi Jinping akitoa hotuba katika uwanja wa Tianmen mjini Beijing.Picha: picture-alliance/dpa/J.Lee

Vifaru, makombora na wanajeshi walipita katika uwanja wa kihistoria wa Tianmen katika gwaride kubwa kukumbuka miaka 70 tangu Japan iliposalimu amri, na kutilia mkazo pia dhamira ya rais Xi Jinping kuifanya China kuwa dola yenye nguvu zaidi katika bara la Asia.

Ili kusisitiza msimamo wa China kwamba kuinukia kwake ni kwa amani na hakutoi kitisho chochote kwa majirani zake, Xi ametangaza kupunguza wanajeshi 300,000 kutoka jeshi la nchi hiyo lenye jumla ya wanajeshi milioni 2.3, ambalo ndiyo jeshi kubwa zaidi duniani.

Gwaride la kijeshi likipita katika uwanja wa Tianmen.
Gwaride la kijeshi likipita katika uwanja wa Tianmen.Picha: Reuters/D. Sagolj

Maendeleo ya amani

''Lazima tujifunze kutokana na historia na tujizatiti katika kudumisha amani. Kwa maslahi ya amani tunahitaji kujenga hisia za jamii ya kimataifa yenye mustakabali shirikishi. Upendeleo, ubaguzi, chuki na vita vinasababisha tu majanga na mateso, wakati kuheshimiana,usawa, maendeleo ya amani na ufanisi wa pamoja vinawakilisha njia sahihi ya kuchukuwa, alisema rais Xi.

Sherehe hizo zimefanyika katika uwanja wa Tianmen, ambako Mao Zedong alitangazia kuundwa kwa Jamhuri ya China mwaka 1949, na zimehudhuriwa na viongozi wa nchi hiyo pamoja na wageni wa heshima, wakiwemo rais wa Urusi Vladmiri Putin, rais wa Korea Kusini Park Geun-hye na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon.

Xi amesisitiza kuwa China itaendelea kujizatiti kwa maendeleo ya amani na kamwe haitatafuta kuitawala dunia au kutanua himaya yake, hata iwe na nguvu kiasi gani, na kwamba haitaisababishia mateso iliyoyapitia nchi nyingine.

Xi ambaye pia ni katibu wa kamati ya uongozi wa chama tawala cha kikomusti na mwenyekiti wa kamisheni kuu ya kijeshi, alikaguwa gwaride la kijeshi lililokuwa na wanajeshi 12,000, zana 500 za vifaa vya kijeshi na ndege za aina mbalimbali, vikiwakilisha kile maafisa wa jeshi walichosema ni teknolojia ya juu zaidi ya kijeshi ya China.

Jeshi likionyesha nguvu yake ya kijeshi wakati wa maadhimisho ya miaka 70 tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya Dunia kwa upande wa Asia.
Jeshi likionyesha nguvu yake ya kijeshi wakati wa maadhimisho ya miaka 70 tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya Dunia kwa upande wa Asia.Picha: picture-alliance/dpa/F. Maohua

Mataifa ya Magharibi yajitenga

Mataifa mengi ya magharibi hayakuwakilishwa na viongozi wake wa juu, hali iliyoakisi wasiwasi kuhusu lugha ya gwaride dhidi ya Japan na hatua za kimabavu za China katika siku za karibuni kudai umiliki wa maeneo ambayo pia yanadaiwa na mataifa mengine.

Marekani ilimtuma tu balozi wake katika sherehe hizo, na mjini Washington, msemaji wa wizara ya ulinzi Bill Urban, alirejelea msimamo wa Marekani kwamba maadhimisho kama hayo yanapaswa kuzingatia zaidi maridhiano, na kwamba maonyesho makubwa ya kijeshi hayaonekani kwenda sambamba na kaulimbiu hiyo.

Japan ilisalimu amri rasmi tarehe mbili Septemba, 1945, na China ilisherehekea ushindi wake siku iliyofuata. Japan ilianzisha uvamizi wa kijeshi kaskazini-mashariki mwa China Septemba 1931, na kufanya uvamizi kamili Julai 7, 1937 wakati majeshi yake yalipofanya shambulizi kwenye daraja la Lugou, pembezoni mwa mji wa Beijing.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,ape

Mhariri: Gakuba Daniel