China yaadhimisha miaka 70 tangu ilipoundwa
1 Oktoba 2019Tunaanzia Beijing mji mkuu wa nchi yenye wakaazi wengi zaidi ulimwenguni China. Nchi hiyo yenye wakaazi zaidi ya bilioni moja na milioni 386, imeingia katika jukwaa la madola makuu ya dunia. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linaimulika jamhuri ya umma wa China na kuandika: "China itaendelea kuangaliwa kama dola lenye nguvu. Hata kama wakoministi madaraka yanawaponyoka, vifungu muhimu vya ufanisi wake vitaendelea kuwepo: yaani idadi kubwa ya wakaazi wake, wafanyakazi walioelimika kupita kiasi, miundo mbinu ya kimambo leo kabisa , kipaji katika masuala ya kiufundi na maarifa katika masuala ya biashara ya dunia. Na hadi wakati huu hakuna ishara ya kuachana na chama cha kikoministi, kinyume kabisa chama hicho ndicho kinachosimamia shughuli za upelelezi, ukandamizaji na propaganda kwa msaada wa teknolojia ya kimambo leo. Miaka 70 baada ya kuundwa kwake, jamhuri ya umma wa China imegeuka kuwa nchi yenye nguvu kupita kiasi. Na inatisha."
Lengo la Wademocrat ni wapiga kura
Marekani inayotambulika rasmi kama dola lenye nguvu kabisa ulimwenguni, inazongwa na mtihani wa ndani. Chama cha Democratic kimeanzisha mchakato wa kumvua madaraka rais Donald Trump, kwa tuhuma za kutumia vibaya madaraka yake. Chanzo, inasemekana amemhimiza rais wa Ukraine ampeleleze mgombea wa kiti cha urais kutoka chama hicho cha Democratic Joe Biden na mwanawe. Gazeti la "Mittelbayerisch Zeitung" linaandika: "Donald Trump hakuwaachia njia nyengine wa Demokrat isipokuwa kutumia jukumu walilopewa kikatiba: yaani kufanya uchunguzi. Spika wa baraza la wawakilishi Nancy Pelosi analitambua hilo vizuri. Wademokrat wanatambua pia kwamba hatimae watakaowazinduwa sio Republican katika baraza la Seneti , bali wapiga kura uchaguzi utakapoitishwa November mwaka 2020. Wakati huo majaji ndio watakaomhukumu rais ambae afadhali angekuwa hajawahi kuingia ikulu ya White House."
Maajabu ya chama cha kihafidhina cha Austria
Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Austria ambako chama cha kihafidhina kimezusha maajabu katika uchaguzi mkuu wa jumapili iliyopita. Gazeti la "Mitteldeutsche Zeiung"linaandika: "Sebastian Kurz alifurahi mno jumapili iliyopita alipojikingia asili mia 5 zaidi ya kura . Jumatatu lakini alianza kutambua, mambo yamegeuka kuwa magumu zaidi. Kabla ya uchaguzi alikuwa na njia tatu za kuchagua: waliberali, wasocial Democrat na walinzi wa mazingira-wote hao walijitokeza kama washirika serikalini. Pindi chama cha siasa kali za mrengo wa kulia kikiamua kukalia viti vya upande wa upinzani, Kurz atabidi ageuze njia. Na kila atakayoifuata itakuwa na changamoto zake ambazo zitakua muhimu kwa mustakbal wa Umoja wa ulaya pia.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir / Inlanadspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga