China na Marekani zalumbana hadharani
19 Machi 2021Maafisa wa ngazi za juu wa Marekani na China wanajiandaa kukutana ijumaa leo baada ya kutofautiana kwa kutoleana maneno makali kwenye mazungumzo yao ya ana kwa ana yaliyofanyika kwa mara ya kwanza tangu rais wa Marekani Joe Biden alipoingia madarakani.
Mazungumzo hayo yalianza siku ya alhamisi ambapo pande hizo mbili zilirushiana maneno makali wakati Marekani iliutuhumu ujumbe wa China kwamba unajinadi kuonesha ushawishi wake kwa lengo la maslahi yake ndani ya China wakati Beijing nayo ikirusha maneno makali vile vile kuelekea Marekani kwa kusema kwamba kuna viashiria vya vita pamoja na mchezo wa kuigiza unaofanywa na Marekani.
Malumbano
Katika matamshi ambayo sio ya kawaida katika mkutano wa kidiplomasia waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken na mkuu wa masuala ya nje wa chama tawala cha China Yang Jiechi walionesha kukosoana kuhusu sera za nje.
Mvutano huu uliojitokeza kwenye matamshi yao ya waziwazi hadharani unaonesha mazungumzo ya faragha huenda yakawa na mjadala mkali zaidi.
Mikutano hiyo inayofanyika Anchorage,Alaska Marekani, inayoendelea kwa vikao vya faragha hii leo Ijumaa ndiyo mtihani mpya katika uhusiano wenye mashaka kati ya China na Marekani ambazo zinakwaruzana kuhusu masuala chungunzima kuanzia biashara hadi haki za binadamu katika jimbo la Tibet ,HongKong,pamoja na jimbo la Xinjiang kadhalika Taiwan na masuala ya mgogoro wa eneo la bahari la kusini mwa China na janga la virusi vya Corona.
Blinken amesema utawala wa rais Biden uko imara na una mshikamano na washirika wake katika kutia msukumo wa kuirudisha nyuma hatua ya China ya kutumia ubabe ndani ya nchi yake na nje.
Lakini kwa upande wa China Yang akaibua msururu wa malalamiko ya nchi yake kuhusu Marekani na kuituhumu Washington kwa unafiki kutokana na kuikosoa Beijing kuhusu suala la haki za binadamu na masuala mengine.
Hata hivyo waziri Blinken aliigeukia tena China na kusema vitendo vya nchi hiyo katika jimbo la Xianjia,HongKong na Taiwan na mashambulizi ya kimtandao dhidi ya Marekani na vitendo vya kulazimisha sera za kiuchumi dhidi ya washirika wa Marekani,ni mambo ambayo sio suala la ndani la China bali ni zaidi ya hapo na ndio sababu Marekani inajiona inawajibika kuyazungumza masuala hayo mbele ya mkutano huo.
Mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan nae akaongeza nguvu kwenye ukosoaji huo kwa kusema China imechukulia vibaya na kuhisi kutukanwa kuhusu masuala ya msingi.
Sullivan akasema Marekani haitaki mgogoro wala kulumbana bali inakaribisha ushindani.
Hata hivyo Yang alihamaki na kuitaka Marekani kuacha kuupigia chapuo mtizamo wake kuhusu Demokrasia katika wakati ambapo hiyo hiyo Marekani yenyewe imekuwa ikikabiliwa na hali ya watu wake kutoridhishwa na mambo yalivyo.
Pia aliishutumu Marekani kwa kushindwa kushughulikia maatatizo yake ya haki za binadamu huku akisema walichokionesha Blinken,Sullivan na maafisa wengine wa Marekani ni kujishusha.
Yang aliongeza kusema kwamba wanaamini ni muhimu Marekani ikabadili mtazamo wa sura yake kwanza na kuacha kukimbilia kuisifia hali yake ya kidemokrasia mbele ya macho ya ulimwengu,wakati ambapo ndani ya Marekani kwenyewe wengi kimsingi wana imani ndogo sana katika demokrasia ya nchi hiyo.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri: Daniel Gakuba