1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Marekani zaigombania Afrika

9 Agosti 2012

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton, amemaliza ziara yake barani Afrika, ambapo alitembelea nchi saba. Clinton alizionya serikali za Kiafrika kuwa makini na washirka wasiosaidia katika maendeleo.

https://p.dw.com/p/15nDX
Waziri Hillary Clinton akiwaSenegal
Waziri Hillary Clinton akiwaSenegalPicha: Reuters

Kauli kali zilisikika kutoka kwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani alipoanza safari yake nchini Senegal. Hillary Clinton alitangaza kwamba serikali ya nchi yake inayasaidia mataifa ya Afrika kuwa na demokrasia zaidi na kusimamia haki za binadamu, na kuongezea kwamba si kila mshirika wa nchi za Kiafrika aliye na lengo hilo. Ilikuwa wazi kwamba Bi Clinton alikuwa akiizungumzia China. Jibu kutoka kwa serikali ya nchi hiyo halikuchelewa: Shirika la habari la China lilisema kwamba nia ya Clinton ilikuwa kuigombanisha China na mataifa ya Kiafrika ambayo yana uhusiano mzuri.

Lakini kuna tofauti gani kati ya sera ya Afrika inayofuatwa na Marekani ikilinganishwa na ile ya China? Ni kweli kwamba Marekani inaweka msisitizo katika juhudi zake za kuboresha demokrasia barani Afrika. Katika sera ya Afrika ya rais Barack Obama wa nchi hiyo, suala la kuwezesha demokrasia linapewa kipaumbele kuliko hata mahusiano ya kibiashara.

Ushindani kati ya China na Marekani waongezeka

China kwa upande wake, haiogopi kuonyesha wazi kwamba haijali sana kuhusu utawala bora au haki za binadamu. Kwa kushirikiana na mataifa mengine yanayounda kundi la BRICS, yaani Brazil, Urusi, India na Afrika Kusini, China inalenga kuweka mfumo tofauti na ule unaofuatwa na watawala wa zamani wa kikoloni. Katika mfumo huo, mataifa ya Magharibi huambatanisha misaada na masharti ya kisiasa. Ingawa China pia inatoa misaada kwa nchi za Kiafrika, haitaki kuingilia katika siasa za ndani za nchi hizo.

Duka linalomilikiwa na mfanyabiashara wa Kichina Senegal
Duka linalomilikiwa na mfanyabiashara wa Kichina SenegalPicha: REBECCA BLACKWELL/AP/dapd

Lakini China na Marekani zinafanana katika jambo moja: nchi zote mbili zinatambua uwezo wa ukuaji wa kiuchumi uliopo Afrika na zinataka kufaidika kutokana na ukuaji huo. Jakkie Cilliers, kutoka taasisi ya masuala ya usalama katika chuo kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini, anafafanua: "Ushindani baina ya Marekani na China katika kugombania soko la barani Afrika unaongezeka. Hivi sasa Afrika imeacha kuwa mahala pa Marekani kupeleka misaada yake tu bali imekuwa mshirika wa muhimu wa biashara."

China yapendelea kulipwa mikopo kwa rasilimali

Utafiti uliofanywa na Umoja wa Ulaya unaonyesha kwamba asilimia 46 ya fedha za misaada zinazotolewa na China hupelekwa Afrika. Mara nyingi fedha hizo hutolewa kwa ajili ya miradi maalum kama vile miradi ya ujenzi wa miundombinu. Miradi hiyo huendeshwa na Wachina wenyewe. Mara nyingi China inapotoa mkopo inataka mkopo huo urejeshwe kwa rasilimali. Mbali na hayo, nchi za Kiafrika zimekuwa soko la muhimu la bidhaa duni kutoka China.

Wahandisi kutoka China wakifanya kazi Sudan Kusini
Wahandisi kutoka China wakifanya kazi Sudan KusiniPicha: picture-alliance/Tong jiang

Philipp Gieg ambaye ni mtaalamu wa masuala ya siasa kutoka chuo kikuu cha Würzburg cha hapa Ujerumani, anafafanua kwamba China si nchi pekee inayofanya biashara isiyo ya haki na nchi za Kiafrika. "Hali ya kutokuwa na usawa kwenye biashara imekuwepo tangu kuanzishwa kwa biashara kati ya watawala wa kikoloni na makoloni yao," anaeleza Gieg. "Zamani rasilimali zilikuwa zikitolewa katika makoloni na badala yake bidhaa za viwandani kurudishwa. Hali hii bado inaonekana katika biashara kati ya Afrika na China, Afrika na Marekani na Afrika na Ulaya."

Mtaalamu huyu anaonya kwamba nchi za Kiafrika lazima ziwe makini kuhakikisha kwamba uwekezaji unaofanywa na mataifa ya nje utakuwa na faida kwa raia. Hata hivyo, mtaalamu huyu anasema kwamba si sawa kuilaumu China kwa uhusiano wake na nchi za Kiafrika.

Mwandishi: Philipp Sandner

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman