1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Marekani katika vita vya kibiashara

23 Machi 2018

Katika mpango wa viwango vipya vya kodi dhidi ya bidhaa kutoka nje ya Marekani,Trump anapanga kuweka  viwango vya ushuru vya juu kabisa hadi dolla bilioni 60 kwa bidhaa za kutoka China,wakati China nayo inachukua hatua

https://p.dw.com/p/2uq7F
USA Washington - Donald Trump verhängt Strafzölle gegen China
Picha: Reuters/J. Ernst

China na Marekani zinalumbana kuhusiana na mgogoro wa kibiashara. Katika mpango huo wa viwango vipya vya kodi dhidi ya bidhaa kutoka nje ya Marekani,Trump anapanga kuweka  viwango vya ushuru vya hadi dolla bilioni 60 kwa bidhaa za kutoka China.

Afisa mmoja wa ngazi ya juu katika utawala wa Marekani ameliambisha shirika la habari la Reuters  ijumaa kwamba Marekani haijatoa kwa  China orodha yoyote ya hatua ambazo inatakiwa kuzichukua ili kuuweka sawa uhusiana wa kibiashara baina ya nchi hizo mbili. Lakini afisa huyo amesema kwamba ikiwa China inataka kuizuia Marekani kuchukua hatua inazopanga kuzichukua za kuongeza maradufu viwango vya ushuru kwa bidhaa zake zinazoingia Marekani basi inatakiwa kuchukua hatua madhubuti za kuibadili hali ya mambo.

China kwa upande wake inasema kwamba inataka kufungua fursa zake za kiuchumi lakini hadi kufikia sasa haijaonekana kuchukua hatua yoyote ya maana kuthibitisha nia yake hiyo, kwa mujibu wa Marekani. Kufuatia mgogoro huo hii leo China imechapisha orodha ndefu ya bidhaa za kutoka Marekani ambazo huenda zikaguswa katika mpango wake mpya wa viwango vya juu vya ushuru ambavyo ni hadi asilimia 25.

Fleischmarkt in Huaibei
Picha: picture-alliance/dpa

Katika orodha hiyo ndefu bidhaa zilizotajwa ni pamoja na nyama ya nguruwe, matunda na mvinyo. Kitisho hicho kilichotangazwa na  China ni hatua ya kulipiza kisasi kutokana na mpango wa sheria mpya za kibiashara uliotiwa saini na rais Donald Trump huko Marekani hivi karibuni ambao pia unalenga kuziwekea bidhaa za China viwango vya juu vya kodi vya hadi asilimia 25. Balozi wa China nchini Marekani Cui Tiankai anasema mgogoro huu hautomsaidia mtu yoyote na badala yake utaleta madhara makubwa kwa wananchi wa kawaida.

''Nafikiri kwamba mwelekeo wa kuchukua uamuzi wa upande mmoja, mtazamo wa kuzuia ushindani wa kibiashara au vita vya kibiashara ni hatua ambazo haziwezi kumsaidia yoyote, kwa sababu haileti maana yoyote kibiashara na wala haina maana kisiasa. Kwa hivyo matokeo ya hatua hizo yatamuumiza kila mmoja. Na bila shaka Wamarekani wanaoishi maisha ya wastani watapata shida. Athari zitaonekana pia katika makampuni ya Wamarekani na hata masoko yake ya fedha. Hatua hii pia itahujumu imani ya wananchi katika maendeleo ya muda mrefu ya kiuchumi. Sifikiri kwamba kuna mtu yoyote atakayefaidika na mgogoro huu.''

Bei za bidhaa za kilimo nchini China zimepanda leo kufuatia vitisho hivyo vya kibiashara kutoka pande zote mbili. Kwa mfano katika soko la mji wa Shenzen, na soko la Guangdong Wenns Foodstuff Group mojawapo ya wafugaji wakubwa wa nguruwe bei zimepanda kutoka asilimia 3.66 hadi Yuan 21.54. Hatua iliyochukuliwa na China kujibu mapigo kuhusu mpango wa Marekani zaidi zimejikita katika bidhaa za kilimo hali ambayo inalenga kutowa fursa nzuri kwa wazalishaji wa ndani kuimarisha bei katika mauzo yao. Kwa upande mwingine hisa katika masoko ya hisa zimeporomoka kwa kasi kubwa.

Wang Qishan Chinas neuer Vizepräsident
Rais Xi Jinping na makamo wake Wang QishanPicha: Reuters/J. Lee

Wizara ya uchumi na biashara ya China imeshaonya kwamba nchi hiyo huenda ikapitisha viwango vya juu vya ushuru katika bidhaa za nyama ya nguruwe kutoka Marekani pamoja na matunda, karanga, mvinyo na mabaki ya mabati ikiwa hakuna maafikiano yatakayopatikana baina ya nchi hizo mbili. Bei za bidhaa mbali mbali za kilimo kutoka Marekani ikiwa ni pamoja na zile zilizoko katika soko kubwa la Hongkong linauza kwa wingi duniani nyama ya nguruwe na ambalo linaagiza nyama hiyo kutoka Marekani zimeporomoka kwa kiwango kikubwa kinachofikia asilimia 5.17. Kwa hivi sasa masoko yanasubiri kuona ikiwa mgogoro huo wa kibiashara wa kulipiziana kisasi kati ya China na Marekani utatanuka na kuziihusisha bidhaa kubwa kama uuzaji wa ndege kutoka Marekani na pia maharage ya soya yanayopelekwa China.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Josephat Charo

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW