China na Japan zazidi kujongeleana
11 Aprili 2007
Ziara hii rasmi ya siku tatu ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa ngazi ya juu wa jamhuri ya umma wa China nchini Japan tangu ile ya waziri mkuu wa zamani Zhu Rongji katika mwaka 2000.
“Nataraji waziri mkuu Wen Jiabao ataikumbuka kwa wema ziara hii” alisema hapo awali mkuu wa serikali ya Japan Shinzo Abe,anaependelea kama anavyosema “kujenga uhusiano wa kimkakati kwa masihali ya pande zote mbili.”
Baada ya mzozo mkubwa wa kidiplomasia ulioshuhudiwa miaka ya nyuma,Tokyo sawa na Beijing watafaidika tuu na hali ya kujongeleana-jambo ambalo wanauchumi wa nchi hizi mbili kila kwa mara wamekua wakilihimiza katika wakati ambapo biashara kati ya nchi mbili na uwekezaji wa moja kwa moja vinaendelea kunawiri.
Katika taarifa ya pamoja iliyotangazwa baada ya mazungumzo hii leo,viongozi hao wawili wa serikali za Japan na jamhuri ya umma wa China,mabwana Wen Jiabao na Shinzo Abe wameelezea azma ya “kutathmini kwa dhati” historia yao-pamoja na kushirikiana katika kuimarisha uhusiano wao kwa masilahi ya kila upande.
“China inahisi Japan inastahiki kuwajibika ndani ya jumuia ya kimataifa” taarifa hiyo ya pamoja imesema,bila ya kutaja lakini moja kwa moja suala la Japan kutaka kua mwanachama wa kudumu wa baraza la usalama.
Hii ni taarifa ya mwanzo ya pamoja kutangazwa hadharani na nchi hizi mbili tangu ziara ya rais wa zamani Jiang Zemin mjini Tokyo katika mwaka 1998.
Viongozi hawa wawili wanatazamiwa pia kutia saini makubaliano ya ushirikiano katika sekta ya nishati ambapo Japan itaipatia China ujuzi na maarifa katika juhudi za kupunguza moshi wa viwandani.
Mad nyengine muhimu mazungumzoni itahusu mzozo wa kinuklea wa Korea ya kaskazini.
Kesho waziri mkuu Wen Jiabao wa China amepangiwa kuhutubia mbele ya bunge-heshma ya aina pekee aliyopewa,kabla ya kukaribishwa na mfalme Akihito na malkia Michiko.
Ijumaa ijayo waziri mkuu wa China atakwenda katika mji mkuu wa kale wa kifalme Kyoto na kuzungumza pamoja na wanafunzi.Atalitembelea pia jiji la Osaka kwa mazungumzo pamoja na wanauchumi.
Muda mfupi kabla ya ziara hiyo kuanza,serikali ya mjini Beijing ilitangaza itaanza upya kuagizia mchele kutoka Japan-shughuli zilizokua zimesitishwa tangu mwaka 2003,eti kwasababu za afya.
Kwa miaka kadhaa sasa nchi hizi mbili zimekua zikizozana na uhusiano wa kibalozi kuzorota Junichiro Koizumi,alipokua waziri mkuu kati ya mwaka 2001 na 2006.
Hata waziri mkuu Shinzo Abe anajulikana pia kwa hisia zake za kizalendo.Alizusha ghadhabu barani Asia alipofifiisha mchango wa japan katika kulazimishwa wanawake wa Asia wageuzwe malaya katika vita vikuu vya pili vya dunia.
Amekwepa lakini hadi wakati huu kusema kama atafuata nyayo za mtangulizi wake au la na kuyazuru makaburi ya Yasukuni.
Kimya hicho ndicho kilichosaidia katika kuimarisha uhusiano pamoja na Jamhuri ya umma wa China.