1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Afrika ya Kusini zaigombania Zimbabwe

Admin.WagnerD22 Novemba 2010

Huku upande mmoja China na Afrika Kusini zikiimarisha uhusiano wao, kwa upande mwengine ziko kwenye kinyang'anyiro cha kuidhibiti Zimbabwe kwa mtazamo wa kunufaika zaidi na maliasili za nchi hiyo, yakiwemo madini

https://p.dw.com/p/QFQU
Rais Jacob Zuma (kushoto) akipeana mkono na mwenzake wa China Hu Jintao wakati wa sherehe ya kusaini mikataba ya mashirikiano kati ya nchi hizi mbili nchini china Agosti 24, 2010
Rais Jacob Zuma (kushoto) akipeana mkono na mwenzake wa China Hu Jintao wakati wa sherehe ya kusaini mikataba ya mashirikiano kati ya nchi hizi mbili nchini china Agosti 24, 2010Picha: AP

Hivi karibuni, Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini alimualika Makamo wa Rais wa China, Xi Jinping, nchini mwake. Jinping ndiye anayetarajiwa kuchukua hatamu ya uongozi nchini mwake na Zuma akatumia fursa hiyo kusaini naye mikataba ya kuboresha biashara baina ya nchi zao, huku China ikionekana kulenga kuwekeza zaidi nchini Afrika ya Kusini.

Lakini unapovuka mpaka na kuingia Zimbabwe, washirika hawa wanatizamana kwa jicho la uhasama. Kwa miaka kadhaa sasa, mataifa hayo mawili yamekuwa yaking'ang'ania kudhibiti na kuwa na usemi zaidi katika uchimbaji wa madini na raslimali nchini Zimbabwe.

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe (kushoto) akikaribishwa na Waziri Mkuu wake Morgan Tsvangirai mbele ya Rais Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini
Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe (kushoto) akikaribishwa na Waziri Mkuu wake Morgan Tsvangirai mbele ya Rais Jacob Zuma wa Afrika ya KusiniPicha: AP

Taifa hilo, lililoko katika kanda ya Afrika Kusini, lilikuwa na usemi mkubwa kutokana na mali asili yake na lilinawiri pia katika sekta ya kilimo kabla ya serikali ya Rais Robert Mugabe kuanza kulivuruga na kusababisha mfumko wa asilimia milioni 500 wa bei kwenye uchumi wake mwaka wa 2008.

Thamani ya mauzo ya bidhaa za Afrika Kusini nchini Zimbabwe ni kama asilimia 20 ya pato la ndani la Zimbabwe. Msaada wa China kwa taifa hilo lililowekewa vikwazo vya kiuchumi kutokana na ukiukaji wake wa haki za binadamu, umemsaidia Rais Mugabe na chama chake tawala cha ZANU-PF kustahimili balaa ya kutengwa na jumuiya ya kimataifa.

China na Afrika ya Kusini zinanuia kudhibiti migodi mikubwa zaidi duniani ya madini ya Platinum inayokadiriwa kuwa yenye thamani ya mabilioni ya Dola, almasi na pia utajiri wa kilimo na pia kuwa na usemi katika hazina ya takriban dola bilioni 10 ya maendeleo ya kulijenga upya taifa hilo baada ya utawala wa rais Mugabe kuisha na sera ya demokrasia kuwepo.

Anne Fruhauf, ambaye ni mchungizi wa masuala ya uchumi katika kundi la Eurasia, anasema mataifa hayo mawili yakilinganishwa kwa sasa, Afrika kusini imejitokeza waziwazi katika maazimio yake ya kiuchumi. Imewekeza katika sekta ya uchimbaji madini na biashara ya benki.

Mataifa mengine ambayo yamekuwa yakilenga kuwekeza na kuidhibiti Zimbabwe kibiashara ni mtawala wake wa zamani, Uingereza, na pia India ambayo kampuni yake ya Essar hivi karibuni ilisaini mkataba wa kuendesha biashara ya kuchonga vyuma wenye thamani ya Dola milioni 500.

Kinyang'anyiro hicho cha udhibiti kinaweza kumpa Bw Mugabe nafasi ya kulipuuza taifa moja na kuliangazia lingine na hatimaye awe na nguvu zaidi ya kuwakashifu wakosoaji wa magharibi na pia kuwakandamiza wapinzani wa ndani wa kisiasa.

Mwezi huu, shirika la fedha duniani, IMF, lilisema mwezi huu kwamba uchumi wa Zimbabwe unaweza ukanawiri kwa mwaka wa pili kwa sababu ya sera mpya na bei thabiti ya bidhaa. China tayari imesaini mikataba ya mabilioni ya fedha ili ishirikiane na Zimbabwe katika sekta ya kilimo, uchimbaji madini, uzalishaji wa nishati na kukarabati miundo mbinu ya taifa hilo iliyosambaratika.

Mugabe alianza kuwa na uhusiano wa karibu na China yamkini miaka 30 iliyopita wakati wa mikakati ya ukombozi na uhusiano huo umekuwa ukinawiri hasa baada ya taifa hilo kutengwa na magharibi.

Makamu huyo wa rais aliondoka Afrika kusini na akaelekea Angola katika kile kinachotajwa na wachunguzi kuwa ni mkakati madhubuti wa kuhakikisha inaendelea kupata mafuta kutoka nchini humo.

Mwandishi: Peter Moss/Reuters

Mhariri: Othman Miraji