China kutokubali kuridhia kupoteza kasi ya maendeleo kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
4 Juni 2007Afisa aliyekuwa akizindua mpango huo amesema kuwa viwango maalum vya udhibiti wa utoaji wa gesi hizo , ambao unazuwia ukuaji wa kiuchumi katika mataifa masikini utakuwa unaathiri zaidi kuliko mabadiliko ya hali ya hewa yenyewe, licha ya kuwa kunatokea maafa ya mvua kali, ukame na kuongezeka kwa kina cha bahari masuala ambayo yanachochewa na kuongezeka kwa ujoto duniani.
Athari zitakazojitokeza kutokana na kupunguza kasi ya maendeleo katika nchi zinazoendelea zitakuwa kubwa zaidi kuliko zile zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa, amesema Ma Kai , mkurugenzi wa maendeleo ya taifa na tume ya mageuzi, ambayo inaendesha sera hii ya mabadiliko ya hali ya hewa.
China haitajifunga kabisa na kiwango cha aina yoyote cha upunguzaji wa gesi hizi , lakini hii haina maan ya kutochukua jukumu la kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa, amewaambia waandishi wa habari.
Mpango wa kwanza wa taifa nchini China juu ya hali ya hewa unapanga kupambana na ongezeko la hali ya joto duniani kwa matumizi bora ya nishati, matumizi mazuri ya ardhi kwa ajili ya kilimo pamoja na kupanda miti.
Lakini waraka huo pia utakuwa kama ngao kwa ajili ya majadiliano makali ya kimataifa yanayofuatia.
Beijing inakabiliwa na miito kadha kutia saini makubaliano ya kuwa na viwango maalum kwa ajili ya kudhibiti utoaji wa gesi zinazoharibu mazingira na kuongeza ujoto katika angani.
Mpango huo umekuja siku mbili kabla rais Hu Jintao kuhudhuria mkutano wa kundi la viongozi wa mataifa manane yenye utajiri mkubwa wa viwanda G8 utakaofanyika nchini Ujerumani ambao utalenga katika matatizo ya kuongezeka kwa hali ya utojo duniani.
Hii ni zaidi ya mkakati maalum wa kujiweka tayari na mapambano wakati mkutano wa mataifa yenye viwanda ukikaribia.
China inataka kuhakikisha kuwa nchi hiyo haitalengwa katika masuala ya ongezeko la ujoto duniani, amesema Wenran Jiang, mtaalamu wa masuala ya nishati katika chuo kikuu cha Alberta.
Mpango huo unaanisha kuwa mataifa tajiri yanatoa gesi hizo kwa wingi zinazopasha joto dunia na bado zinatoa gesi hizo kwa wingi kwa kiwango cha kila mtu kuliko China, kwa hiyo mataifa hayo yanapaswa kutoa fedha kwa ajili ya kupata maendeleo katika usafi wa mazingira, badala ya kuyalazimisha mataifa masikini kukubaliana na viwango vya utoaji wa gesi hizo.
Mataifa tajiri yamehamishia uzalishaji wa bidhaa zao katika masikini kama China na sasa yanayalaumu mataifa hayo kwa kuchafua mazingira, wakati wao wanaburuza miguu juu ya ahadi za kugawana teknolojia safi ambayo haiharibu mazingira, amesema Jiang.
Tunahisi kuwa kumekuwa na ngurumo nyingi lakini mvua kidogo, mazungumzo mengi lakini hatua hakuna, amewaambia waandishi wa habari wakati akiulizwa iwapo China inaridhika na uhamishaji wa teknolojia .
Ma amesema katika mwaka 2004 kiwango cha wastan cha utoaji wa gesi hizo kwa kila mtu nchini China ni kiasi cha moja ya tano ya viwango vya Marekani kwa mwaka.
Mvutano kuhusu gesi zinazoharibu mazingira unaongezeka wakati majadiliano yatakapoanza juu ya kurefusha makubaliano ya umoja wa mataifa ya Kyoto kupindukia 2012, wakati makubaliano ya awamu ya kwanza ya Kyoto yaliyoanza mwaka 1997 yatakapomalizika.