1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China, Japan na Korea Kusini zataka amani Rasi ya Korea

9 Mei 2018

Viongozi wa China, Japan na Korea Kusini wamekubaliana kushirikiana kuitafuta amani katika Rasi ya Korea na kuunga mkono juhudi za kidiplomasia kuitaka Korea Kaskazini kuachana na mpango wake wa silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/2xQ6x
Südkorea, Japan und China beraten über Nordkorea
Picha: Getty Images/AFP/E. Hoshiko

Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in, Waziri Mkuu wa China Li Keqiang na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, wamekubaliana kushirikiana wakati ambapo Korea Kusini na Korea Kaskazini zinaelekea katika mchakato wa kupatikana kwa amani ya kudumu. Viongozi hao wanahudhuria mkutano wa pande tatu unaofanyika mjini Tokyo, Japan. Mkutano wa mwisho wa aina hiyo ulifanyika mwaka 2015 mjini Seoul, Korea Kusini.

Korea Kaskazini ilihodhi katika mkutano huo, baada ya mkutano wa kihistoria kati ya Moon na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un mwezi uliopita. Abe mwenyeji wa mkutano huo amezipongeza juhudi za China na Korea Kusini na hatua ya kuweka kando tofauti zao katika kufanikisha amani kwenye Rasi ya Korea.

Amani kwenye Rasi ya Korea

Kwa upande wake Moon amesema viongozi hao wamekubaliana kuhusu matokeo ya mazungumzo kati ya Korea hizo mbili ya kuondoa kabisa silaha za nyuklia katika Rasi ya Korea na kuanzisha uhusiano mzuri na kuhakikisha amani inapatikana.

''Tumekubaliana kuhakikisha tunaondoa silaha za nyuklia kwenye Rasi ya Korea, panakuwa na amani na maendeleo katika uhusiano kati ya nchi hizi mbili kwa ajili ya ustawi wa Rasi ya Korea na nchi za Kaskazini Mashariki mwa Asia,'' alisema Moon.

Südkorea TV Trump Kim Jong Un
Televisheni ikionyesha picha ya Trump, Moon na KimPicha: picture-alliance/AP/A. Young-joon

Viongozi wa mataifa hayo matatu yenye nguvu barani Asia, ambao uhusiano wao wakati mwingine uligubikwa na mzozo wa kikanda na kihistoria pia wamejadiliana masuala ya kiuchumi katika wakati ambao Rais wa Marekani Donald Trump ameongeza shinikizo la kibiashara kwa China na Japan.

Pia wamekubaliana kwamba Korea Kusini na China zinaweza kuanza kufanya utafiti wa pamoja kuhusu uwezekano wa kuwepo miradi ya reli itakayoziunganisha nchi hizo mbili.

Mustakabali wa Korea Kaskazini

Aidha, Moon na Keqiang wamesema Korea Kaskazini inapaswa kupewa msaada wa kiuchumi kama kweli itaachana kabisa na mpango wake wa silaha za nyuklia. Viongozi hao wamekubaliana kwamba jumuiya ya kimataifa ikiwemo Marekani zinapaswa kuihakikishia Korea Kaskazini mustakabali mzuri, kama vile usalama wa serikali na maendeleo ya kiuchumi.

Mkutano huo pia ni sehemu ya maandalizi ya mkutano wa kilele kati ya Marekani na Korea Kaskazini unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo yuko mjini Pyongyang na amekutana na maafisa wa ngazi ya juu wa Korea Kaskazini kwa lengo la kukamilisha maandalizi ya mkutano wa Trump na Kim.

Baada ya mazungumzo hayo, Pompeo amewaambia waandishi habari kwamba wanategemea kukubaliana kuhusu tarehe na sehemu utakapofanyika mkutano huo. Hata hivyo kuna taarifa kwamba huenda ziara hiyo ya Pompeo pia ikasaidia kuachiliwa huru kwa raia watatu wa Marekani wanaoshikiliwa Korea Kaskazini.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, Reuters
Mhariri: Saumu Yusuf