1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China inaweza kuinyamazisha Korea Kaskazini?

Saumu Ramadhani Yusuf7 Desemba 2010

Marekani,Korea Kusini na Japan zajadiliana kuhusu uchokozi wa Korea Kaskazini

https://p.dw.com/p/QRfA
Mawaziri wa Mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton, Japan, Seiji Maehara,na Korea Kusini Kim Sung-hwanPicha: AP

Katika mzozo wa Korea unaondelea,China hii leo imepuuza ripoti ya Marekani inayoishutumu nchi hiyo kwa kuipa nguvu Korea Kaskazini ya kuanzisha urutubishaji wa madini ya Uranium na kuanzisha tena mashambulio dhidi ya jirani yake Korea Kusini.China imesema madai hayo hayana msingi.Matamshi hayo ya China yamekuja baada ya hapo jana kufanyika mazungumzo ya pande tatu huko Washington kati ya mawaziri wa nje wa Marekani,Korea Kusini na Japan kuhusu suala hilo la Korea Kaskazini.

Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi hizo Tatu wote walikuwa na msimamo mmoja kuelekea msimamo wa Uchokozi wa Korea Kaskazini dhidi ya jirani yake Korea Kusini na wameitaka China ambayo ni rafiki wa karibu wa nchi hiyo ya kikomunisti kuchukua hatua zaidi katika kuibadili tabia ya Korea Kaskazini.Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton,Seiji Maehar wa Japan na Kim Sun Hwan wa Korea Kusini walianza kwa kukaa kimya kwa dakika moja kwa ajili ya kuwakumbuka wahanga wa Korea Kusini.

NO FLASH nordkoreanischen Beschuss der südkoreanischen Insel Yonpyong
Uchokozi wa Korea Kaskazini wazitia wasiwasi nchi za MagharibiPicha: AP

Waziri huyo wa mambo ya nje wa Marekani pia anasema mashambulio ya Korea Kusini ya hivi karibuni yanafuatia mlolongo wa visa vya uchokozi vilivyowahi kushuhudiwa huko nyuma.Amekumbusha juu ya mashambulio ya makombora yaliyofyatuliwa na nchi hiyo mnamo mwezi marchi mwaka huu dhidi ya nyambizi ya Korea Kusini na kusababisha vifo vya wanajeshi 46,wakati ambapo nchi hiyo ilikuwa imeshatoa nafasi kwa mwanasayansi wa Kimarekani kukitembelea kinu chake cha kurutubisha madini ya Uranium. China imetoa mwito wa kurudi tena kwa mazungumzo maalum ya pande sita juu ya mpango wa Nuklia wa Korea Kaskazini lakini mawaziri hao watatu wa mambo ya nje kwa mujibu wa Clinton wamekataa pendekezo hilo la China.

Katika mazungumzo hayo ya pande sita pia zinahusika China Urusi na Korea Kaskazini yenyewe.Kabla ya mkutano huo wa Jana rais Barack Obama alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na mwenzake wa China Hu Jintao,na kuitaka China kushirikiana na Marekani katika kuutatua mzozo huo wa Korea na kwamba China ipeleke mjumbe wake Korea Kaskazini kuikanya nchi hiyo kuhusu vitendo vyake visivyokubalika.Lakini China imeshatoa onyo kwa pande zote mbili kujizuia kufanya uchokozi na kusababisha kuharibu hali ya mambo katika eneo hilo.

Mwandishi Bergmann Christina ZR/Saumu Mwasimba

Mhariri Abdul-Rahman