China haikuridhishwa na maamuzi yaliyochukuliwa na Ujerumani
1 Agosti 2020Katika taarifa kwenye wavuti yake, ubalozi wa China amesema kusimamishwa kwa mkataba huo, Ujerumani imekiuka sheria za kimataifa pamoja na sheria za kanuni ya msingi wa uhusiano wa kimataifa, na kwamba ni dhahiri kuwa Ujerumani inaingilia kati maswala ya ndani ya China. Ubalozi wa China umeonyesha kutoridhika na kauli iliyotolewa na waziri wa mamo ya nje wa Ujerumani heiko Maas ubalozi huo umesema kwamba China ina haki ya kujibu juu ya hatua zilizochukuliwa na Ujerumani laki ya kufafanua zaidi.
Waziri wa Mambo ya nje wa Ujerumani Heiko Maas alisema siku ya Ijumaa kwamba nchi yake itasimamisha kwa muda utekelezaji wa mkataba, baina ya Ujerumani na Hong Kong unaowezesha wahalifu wa kila upande kurudishwa kwao. Maas pia alisisitiza kwamba Ujerumani wakati wote inatarajia kuwa China ambayo imetangaza sheria mpya ya usalama wa taifa mjini Hong Kong itatekeleza wajibu wake wa kimataifa.
Ujerumani imesimamisha makubaliano hayo kati yake na Hong Kong baada ya kiongozi wa Hong Kong kuahirisha uchaguzi wa bunge uliokuwa ufanyike Septemba 6 ambapo Maas amesema uamuzi wa serikali ya Hong Kong wa kuwakatalia wajumbe 12 wa upinzani kugombea katika uchaguzi huo ni ukiukaji mwingine wa haki za raia wa Hong Kong.
Wajumbe hao ni pamoja na kiongozi wa harakati za kidemokrasia Joshua Wong amaye ameeleza kuwa serikali ya China inachukua hatua mbalimbali kwa lengo la kuwazuia wapinzani kushinda viti vingi bungeni. Maas amesisitiza kwamba Ujerumani wakati wote inatarajia kuwa China ambayo imetangaza sheria mpya ya usalama wa taifa mjini Hong Kong itatekeleza wajibu wake wa kimataifa.
Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam ametangaza kuahirishwa uchaguzi wa bunge, ameleeza kwamba uchaguzi huo umeahirishwa kutokana na kuongezeka kwa maambukizi ya virusi vya corona.
Vyanzo: RTRE/DPA