1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chelsea yaiondoa Liverpool kileleni

21 Novemba 2016

Chelsea iliiondoa Liverpool kileleni mwa Ligi ya Premier ya England, baada ya kuifunga Middleborough  bao moja kwa sifuri Jumapili (20.11.2016)

https://p.dw.com/p/2T1X3
Fußballer Diego Costa und Eden Hazard (FC Chelsea)
Picha: picture-alliance/dpa/F. Arrizabalaga

Ulikuwa ushindi wao wa sita mfululizo na kuwapa pointi 28, moja mbele ya Liverpool ambao walitoka sare tasa na Southampton. Yaya Toure alirejea katika kikosi cha Manchester City kuifungia mabao mawili katika ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Crystal Palace. City pia wana pointi 27 sawa na Liverpool. Arsenal ilitoka sare ya 1-1 na Manchester United na kubakia katika nafasi ya nne na pointi 25 moja mbele ya Spurs wanaofunga tano bora.

Kule Uhispania, Real Sociedad ilisonga hadi nafasi ya tano baada ya ushindi wao wa nne mfululizo dhidi ya Sporting Gijon wa mabao 3-0. Waliwaruka Atletico Madrid ambao walizabwa 3-0 na Real Madrid mabao yote yakifungwa na CR7. Barca wanawafuata viongozi Real Madrid na pengo la pointi nne baada ya kukabwa sare tasa dhidi ya Malaga.

Katika Serie A ya Italia, Inter Milan ilitoka sare ya 2-2 na AC Milan katika derby ya kusisimua. AC Milan ilidhamiria kupanda hadi nafasi ya pili nyuma ya JUuventus baada ya Roma kuzabwa 2-1 na Atalanta lakini mambo yakaharibiwa na Ivan Perisic

sekunde chache kabla ya mchuano kukamilika. Sasa AC Milan wanabakia katika nafasi ya tatu pointi sawa na Roma, wote wakiwa nyuma ya viongozi Juventus na pengo la pointi saba. Inter wamesonga juu hadi nafasi ya 9.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef