Chavez azikwa
8 Machi 2013Marais na viongozi 55 wa nchi kadhaa wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya Chavez wakiwemo rais wa Cuba Raul Castro, rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad,rais wa Brazil Dilma Rousseff na wa Belaruss Alexander Lukashenko miongoni mwa wengine wengi.
Mrithi wake kisiasa makamu wa rais wa taifa hilo Nicolas Maduro ameahidi kuuhifadhi mwili wa Chavez ambaye sera zake za kisosholisti ziliwapendeza mno masikini na kuwaudhi matajiri wa taifa la Venezuela ili usioze kama ulivyofanyiwa mwili wa aliyekuwa kiongozi wa mrengo wa kushoto Lenin na kuwekwa kwenye jeneza la glasi ili uonekane milele.
Maduro kuapishwa leo
Spika wa bunge nchini humo Diosdado Cabello amesema baada ya mazishi hayo ya kitaifa ya Chavez hii leo, Maduro anatarajiwa kuapishwa rasmi kama rais wa muda wa taifa hilo kabla ya kuitishwa uchaguzi. Baraza la kitaifa la uchaguzi lina jukumu la kuweka tarehe ya uchaguzi wa urais ambao sharti uitishwe katika kipindi cha siku thelathini zijazo kuambatana na katiba.
Mwili wa Chavez baadaye utapelekwa katika kambi ijulikanyo kama Mountain Barracks ambayo kwa sasa imebadilishwa kuwa jumba la makumbusho ya harakati za ukombozi wa taifa hilo. Ni katika kambi hiyo ya kijeshi ambapo Chavez alianzisha jaribio lilotibuka la kuipindua serikali ya Carlos Anres Perez mnamo tarehe 4 mwezi Februari mwaka 1992. Kukamatwa kwake baada ya kutibuka kwa jaribio hilo ndiko kulikomfanya shujaa na kumpa ushindi katika uchaguzi wa mwaka 1998.
Huku hali ya kisiasa ikionekana kuwa tete kutokana na kifo cha Chavez,Maduro ametangaza kuwa muda wa umma kuuona mwili wa kiongozi huo umeongezwa kwa siku nyingine saba baada ya sherehe za mazishi yake leo. Serikali imesema zaidi ya watu milioni mbili kutoka kila pembe ya taifa hilo wamekuja kuutizama mwili wake tangu Jumatano.
Wasiwasi baada ya Chavez
Chavez ambaye aliugua saratani kwa karibu miaka miwili amefariki akiwa na umri wa miaka 58 na wengi wa raia wa taifa hilo wameingiwa na wasiwasi kuhusu kama mrithi wake ataweza kulidhibiti taifa hilo lenye utajiri mkubwa wa mafuta na kuendeleza sera zake zilizoonekana kuwapa afueni watu wa kiwango kidogo cha mapato na mataifa jirani hasa Cuba.
Maduro aliye na umri wa miaka 50 anatarajiwa kumenyana katika kinyang'anyiro cha urais na kiongozi wa upinzani nchini humo Henrique Capriles aliyeshindwa na Chavez mwezi Oktoba mwaka jana.
Mwandishi: Caro Robi/AFP
Mhariri: Saumu Yusuf