Chavez ashinda tena urais
8 Oktoba 2012"Idumu Venezuela. Adumu mwasisi Bolivar. Yadumu Mapinduzi ya Bolivar!" Rais Chavez alijitokeza kwenye roshani kuwasilimia maelfu ya wafuasi wake waliokusanyika nje ya kasri ya rais mjini Caracas kushangiria ushindi wa asilimia 54 wa kiongozi huyo mwenye siasa kali za mrengo wa shoto.
Dalili kwamba Chavez angelishinda tena uchaguzi huu zilikuwa zimeanza mapema hata kabla ya Tume ya Uchaguzi kutangaza rasmi matokeo. Wafuasi wake tayari walikuwa wamejazana mitaani, wakishangiria kwa kurusha fashifashi na kupiga mayowe ya "Idumu Venezuela. Adumu Chavez!"
Hata hivyo, wagombea wote wawili walikuwa wameshaonesha kukubaliana na matokeo ya uchaguzi huo vyovyote yatakavyokuwa. Rais Chavez aliwataka wafuasi wake kutulia na kukubali matokeo yoyote yatakayotangazwa.
Capriles akiri kushindwa
Naye Henrique Capriles, aliyeendesha kampeni zilizotoa upinzani mkali wa Chavez, amekiri kushindwa na kumpongeza Rais Chavez.
"Anayejua kushinda anaweza pia kushindwa. Mimi ni mwanademokrasia. Nautambua uamuzi wa umma. Nauheshimu uamuzi huo. Na nampongeza rais wa Jamhuri!" Amesema Capriles.
Katika hotuba yake kwa umma mara tu baada ya kuthibitishwa ushindi, Rais Chavez ameahidi kufanya kazi na upinzani huku akitoa wito wa kuwapo umoja wa kitaifa katika nchi hiyo iliyogawika.
Chavez amesema licha ya kuwa ushindi wake ni wa wazi na kamili, bado anahitaji kumshirikisha "kila mtu kwenye uongozi wakiwemo wapinzani."
Chavez kuendeleza usoshalisti
Hata hivyo, amewaambia wafuasi wake kwamba ataendelea na sera zake za mapinduzi kuelekea usoshalisti wa kidemokrasia katika karne ya 21 na kuahidi kuwa rais bora zaidi ya vile alivyokuwa katika siku za karibuni.
Ushindi huu wa Chavez, aliyeingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 1998, unamfanya kuwa kiongozi pekee katika Marekani ya Kusini kuhudumu muda mrefu kutokana na kura za wananchi.
Tayari viongozi wenzake wa eneo hilo wameanza kutuma salamu za pongezi, wakisema huo ni ushindi si kwa Chavez tu bali kwa washirika wote wa Marekani ya Kusini.
"Ushindi wa Rais Chavez ni ushindi kwa demokrasia. Sio tu ni ushindi wa kwa watu wa Venezuela. Ni ushindi kwa umoja wa Bolivar na kwa Marekani ya Kusini yote." Amesema Rais Evo Morales wa Bolivia katika salamu zake.
Maneno kama hayo yamesema pia na Rais Rafael Correa wa Equador, ambaye kwenye mtandao wa Twitter ametuma ujumbe unaosomeka: "Idumu Venezuela, adumu baba wa taifa, yadumu mapinduzi ya Bolivar!"
Kwa ushindi huu wa sasa, Chavez mwenye miaka 58 na anayedai kuyashinda maradhi ya saratani, atabakia madarakani mpaka mwaka 2009, muda unaotosha kuyaimarisha yale yanayoitwa "Mapinduzi ya Bolivar!" yanayochimbukia kwa Simon Bolivar, kiongozi wa karne ya 19 wa harakati kadhaa za ukombozi katika mataifa kadhaa ya Amerika ya Kusini.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/DPA
Mhariri: Saumu Yusuf