1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Charles III atangazwa rasmi kuwa mfalme wa Uingereza

10 Septemba 2022

Mfalme Charles III ametangazwa rasmi kuwa mfalme wa Uingereza katika hafla ya kihistoria iliyofanyika kwenye kasri la Mtakatifu James, jijini London.

https://p.dw.com/p/4GfSO
Großbritannien London | Proklamation König Charles III.
Picha: Jonathan Brady/AP Photo/picture alliance

Baraza la Viongozi lenye jukumu la kumtangaza mfalme, lilimtangaza rasmi Mfalme Charles III  siku ya Jumamosi na hafla hiyo imeoneshwa moja kwa moja katika televisheni ikiwa ni kwa mara ya kwanza. Baraza hilo linaundwa na wanasiasa wa ngazi ya juu na maafisa ambao wanamshauri mfalme.

Baraza hilo lilikutana kabla, bila ya Charles kuwepo wakati linatangaza rasmi jina la mfalme mpya kama mkuu wa nchi kuwa ni Mfalme Charles III.

Charles, mwenye umri wa miaka 73, mtoto mkubwa wa Malkia Elizabeth II alichukua kiti cha ufalme moja kwa moja mara tu baada ya kifo cha mama yake Malkia Elizabeth II, kilichotokea Septemba 8, na hafla ya kutangazwa rasmi Jumamosi ni hatua muhimu ya kikatiba na uthibitisho wa utambulisho wake kama mfalme mpya wa Uingereza.

Charles III. wird feierlich zum König proklamiert
Mfalme Charles III akisaini kiapo mbele ya mkewe, Camilla na mwananawe Mwanamfalme WilliamPicha: Victoria Jones/dpa/picture alliance

Baada ya kutangazwa rasmi, Mfalme Charles III, aliungana na wajumbe wa baraza hilo na kula viapo kadhaa na kukiri matamko. Baada ya hapo Mfalme Charles III alitangaza rasmi kifo cha mama yake, Malkia Elizabeth wa Pili, aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 96.

Katika hotuba yake Mfalme Charles III aliushuruku umma kwa kuwa pamoja na familia yake yote baada ya msiba huo. Amesema anafahamu kwa kina "majukumu mazito" ambayo amepewa kama mtawala mpya.

Mfalme asema ataiga mfano wa mama yake

"Katika kuchukua majukumu hayo nitajitahidi kuiga mfano wa kutia moyo wa mama yangu katika kufuata na kudumisha katiba na kutafuta amani, maelewano na ustawi wa watu wa visiwa hivi, na ulimwengu wa jumuia ya madola duniani kote," alisema Mfalme Charles III.

Pia alimshuruku mkewe, Camilla kwa msaada ambao amekuwa akimpa mara kwa mara. Kama ilivyo utamaduni, Mfalme Charles III pia alikula kiapo cha kudumisha usalama wa Kanisa la Scotland.

Mfalme Charles III alisindikizwa katika hafla hiyo na mkewe, Camilla pamoja na mtoto wake mkubwa Mwanamfalme William. William sasa ndiye mrithi wa kiti cha ufalme na anajulikana kama Mwanamfalme wa Wales, cheo ambacho kimekuwa kikishikiliwa na Charles kwa takribani miongo mitano.

Hii ni mara ya kwanza hafla hiyo inafanyika tangu mwaka 1952, wakati Malkia Elizabeth II alipotangazwa kuwa malkia wa Uingereza.

Großbritanien I Charles III. wird feierlich zum König proklamiert
Kiongozi wa chama cha Labour, Keir Starmer akiwa na mawaziri wakuu wastaafu, Tony Blair, Gordon Brown na Boris JohnsonPicha: Kirsty O'Connor/AP/picture alliance

Miongoni mwa viongozi wa Uingereza waliohudhuria hafla hiyo ni pamoja na Waziri Mkuu mpya wa Uingereza, Liz Truss, pamoja na mawaziri wakuu wa zamani w anchi hiyo Tony Blair, David Cameron na Boris Johnson. Kiongozi mwengine wa kisiasa aliyehudhuria ni mkuu wa chama cha upinzani cha Labour, Keir Starmer.

Waziri Mkuu wa Uingereza ala kiapo cha utii kwa Mfalme Charles III

Waziri Mkuu wa Uingereza, Liz Truss na maafisa wa ngazi ya juu wa serikali yake, wamekula viapo vya uaminifu kwa Mfalme Charles wa III katika Bunge la Uingereza, saa chache baada ya Charles kutangazwa rasmi kuwa mfalme wa Uingereza.

Spika wa Bunge, Lindsay Hoyle alikuwa wa kwanza kuahidi kuwa mtiifu wa kweli kwa Mfalme Charles, mrithi wake na warithi wake. Hoyle alifuatiwa na wabunge waliokaa muda mrefu zaidi na Waziri mkuu.

Wabunge wote wanaapa kumtii mfalme pindi wanapochaguliwa. Hata hivyo, kuapa upya wakati utawala wa kifalme unapobadilika sio lazima kisheria, lakini wabunge wote 650 watakuwa na nafasi ya kuapa upya katika siku zijazo kama watapenda kufanya hivyo.

Großbritannien | Tod Queen Elizabeth | Premierministerin Liz Truss
Waziri Mkuu wa Uingereza, Liz TrussPicha: House of Commons/AP Photo/picture alliance

Bunge la Uingereza Jumamosi linafanya kikao kisicho cha kawaida ili kuwaruhusu wabunge kumuenzi Malkia Elizabeth wa II. Shughuli nyingine zote za bunge zimesitishwa baada ya kifo cha Malkia.

Aidha, Rais wa Urusi, Vladmir Putin amempongeza Mfalme Charles III kwa kutangazwa rasmi kuwa mfalme wa Uingereza. Ubalozi wa Urusi mjini London umeandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba Rais Putin amemtakia mfalme huyo afya njema na kila la kheri.

Wakati huo huo, safari ya kumpumzisha Malkia Elizabeth II katika nyumba yake ya milele itaanza rasmi. Mfalme Charles III ametangaza kuwa siku ya mazishi ya mama yake itakuwa siku ya mapumziko.

Charles aliidhinisha uamuzi huo wakati wa kutangazwa kwake Jumamosi. Hata hivyo, tarehe rasmi ya mazishi ya kitaifa ya Malkia Elizabeth II haijatangazwa rasmi, lakini inatarajiwa kuwa Septemba 19.

Viongozi mbalimbali kuhudhuria mazishi ya Malkia

Mfalme Naruhito wa Japan, anapanga kusafiri kwenda Uingereza kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II katika kile kinachoelezwa kuwa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipotawazwa kuwa mfalme Mei 2019.

Japan Zehntausende feiern Thronbesteigung von Kaiser Naruhito
Mfalme Naruhito wa Japan akiwa na mkewe, MasakoPicha: picture-alliance/AP Photo/E. Hoshiko

Duru za serikali ya Japan zimeeleza kuwa nchi hiyo pia inaandaa mipango ya mke wa Naruhito, Masako kumsindikiza mumewe iwapo atapenda kufanya hivyo.

Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida pia huenda akahudhuria mazishi hayo, yanatotarajiwa kufanyika jijini London katika jumba la Westminster Abbey.

Rais wa Marekani, Joe Biden pia amesema atakwenda Uingereza kuhudhuria mazishi ya Malkia Elizabeth II, ingawa hajaeleza kwa undani kuhusu ziara yake hiyo.

(AP, AFP, Reuters)