1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chanzo cha mzozo wa Lebanon ni kipi?

Maja Dreyer22 Mei 2007

Mapigano yanaendelea nchini Lebanon – na ndilo suala linalozungumziwa pia na wahariri wa humu nchini.

https://p.dw.com/p/CHSu

Kwanza ni gazeti la Badische Zeitung ambalo linatafuta chanzo cha mzozo huu:

“Katika mapigano haya mapya, kwa mara nyingine tena ni vigumu kusema nani ana maslahi gani na huenda makundi au nchi gani za nje zina mahusiano yapi nchini Lebanon. Serikali ya Lebanon inailaumu Syria kwa kuvunja utulivu kupitia msaada wa Waislamu. Huenda ni kweli. Lakini kile ambacho hakina mantiki ni lawama ya Lebanon kwamba Waislamu hawa walioanza ghasia ni wa kundi la Al-Qaida, kwani magaidi wa al-Qaida, bila shaka, si marafiki za serikali ya Syria. Jambo ambalo tunaweza kusema kwa hakika ni kwamba nchini Libanon kuna makundi mengi mno ya kisiasa na ya kidini ambayo yana malengo tofauti. Kwa hivyo ni vigumu sana kuamini makundi haya yote yataweza kuendesha nchi kwa pamoja.”

Ni uchambuzi wa “Badische Zeitung”. Anayejaribu pia kufahamu mzozo wa Libanon ni mhariri wa “Südwest Presse”. Ameandika:

“Huwezi kuielewa nchi ya Lebanon kabla hujaizingatia Syria ambayo bado imekasirika kutokana na kulazimishwa kuondosha jeshi lake kutoka Lebanon. Kwa Syria, Lebanon ni kama mkoa wake. Inataka kuvurugu amani ya nchi hiyo, kwani ikiwa kutakuwa na ghasia, pande moja husika ya Lebanon itaenda Syria kuomba msaada. Nani tena aliwapatia silaha wale walioanza ghasia hizo? Lakini chanzo cha hali hiyo nzima ni suala la Wapalestina ambalo bado halikutatuliwa. Lebanon inaweza kuwa na usalama tu wakati makambi ya wakimbizi yatakapofungwa.”

Na hatimaye juu ya suala la mizozo inayoendelea Mashariki ya Kati, hilo hapa gazeti la “Berliner Zeitung”:

“Ulafi wa kupata mafuta na maslahi ya kimkakati ya nchi za Magharibi katika eneo la Mashariki ya Kati, hatua za kuingilia kijeshi katika mamlaka ya nchi, hivi ndivyo vyanzo vya mizozo mingi. Na mizozo inaendelea kwa sababu kuyaunga mkono mamlaka fulani ya kidikteta, vile vile kutokana na kuwa na mipango mibaya ya amani, kama mfano wa kulazimisha demokrasia kwa njia ya kivita.”

Haya ni maoni ya mhariri wa “Berliner Zeitung”. Tukielekea sasa gazeti la “Handelsblatt” la kutoka Düsseldorf, mhariri wake anazungumzia juhudi za kundi la nchi zinazostawi kiviwandi dunuani, G8, kuongeza msaada wake kwa mataifa ya kiafrika. Gazeti limeandika:

“Fedha pekee hazitatatua matatizo yaliyopo barani Afrika. Ni jambo la kupongeza kuwa kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, anataka kuwakumbusha viongozi wengine wa kundi la nchi za G8 kutekeleza ahadi walizotoa kwenye mkutano wa Gleneagles miaka miwili iliyopita ya kuongeza kwa mara mbili msaada wao kwa bara la Afrika. Lakini msaada wa kiserikali si dawa mjarab kwa maradhi yote. Inabidi serikali zote, mashirika ya kimataifa na sekta ya uchumi zishirikiane kutafuta suluhisho. Hasa makampuni yanaweza kuchangia vikubwa kwa kutega uchumi, kwani kinachohitajika hasa barani Afrika ni ajira.”