Chanjo nyingine ya Covid-19 yaanza kutumika Kenya
31 Machi 2021Wakati huo huo, zoezi la kuwapa wahudumu wa afya mafunzo linaendelea kwa azma ya kuhakikisha chanjo salama zinayowafikia watu wengi zaidi nchini humo.
Chanjo ya Sputnik V inayotengenezewa nchini Urusi inapatikana nchini Kenya na ubalozi wa Urusi nchini Kenya umethibitisha kwamba iliingizwa na chombo cha kibinafsi kwa kusudi la kibiashara. Kadhalika, kupitia taarifa rasmi ubalozi huo umesisitiza kuwa walio iagiza chanjo hiyo lazima wafuate masharti yote yaliyotolewa na mamlaka ya Kenya.
Wanasheria wawili maarufu wa Kenya wameshiriki chanjo.
Tayari mawakili wawili maarufu wamethibitisha kuwa wamechanjwa chanjo hiyo ya Sputnik V. Wakionyesha picha za shughuli yenyewe kwenye mitandao ya kijamii, wameelezea imani yao katika uwezo wa chanjo hiyo kuwakinga na maambukizi yote ya ugonjwa wa COVID 19. Wizara ya afya nchini imepinga matumizi ya chanjo hiyo, wanayosema kwamba bado haijaidhinishwa.
Dokta Mercy Mwangani, ni afisa msimamizi katika wizara ya afya amenukuliwa na vyombo vya habari akisema "Tumepokea taarifa kuhusu kuingia nchini kwa chanjo ya Urusi ya Sputnik V. Tunajua pia kwamba mkataba wa makubaliano unaoeleza majukumu ya kila anayehusika katika usambazaji wa chanjo hiyo haujawasilishwa kwenye bodi ya wafamasia. Hii inamaanisha kwamba chanjo hiyo haijapokea idhini inayohitajika ili iweze kutumika nchini.” alisema afisa huyo.
Kampuni inayotoa chanjo ya Sputnik V inataka kuruhusiwa kuuza chanjo hiyo nchini kama chanjo ya dharura. Haya yanajiri wakati kaunti mbalimbali zinaendeleza mafunzo kwa wahudumu wake wa afya nchini ili kuwapa ujuzi zaidi na kuhakikisha usalama wa chanjo ya Astrazeneca inayotolewa na serikali ya Kenya.
Ubalozi wa Urusi nchini Kenya umabainisha kwamba maswali yote yanayohusu uagizaji binafsi wa chanjo ya Sputnik V nchini Kenya yanapaswa kuulizwa watu walioiingiza nchini.
Chanzo: DW Nakuru