1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto Baada ya Uchaguzi wa Bunge la Ulaya

27 Mei 2014

Uchaguzi wa bunge la Ulaya na ule wa Ukraine ndizo mada zilizohanikiza magazetini yakichomoza matumaini ya kukutana katika meza ya majadiliano mahasimu wawili wakuu wa Ukraine

https://p.dw.com/p/1C7V0
Ramani ya nchi 28 za Umoja wa Ulaya

Tunaanzia lakini Brussels ambako viongozi wa mataifa 28 ya Umoja wa Ulaya wanakutana kutafakari kiu cha mageuzi cha wapiga kura wa Ulaya. Mageuzi yanahitajika na ukweli huo viongozi wameanza kuutambua. Lakini kutokana na matokeo ya uchaguzi wa bunge la Ulaya yaliyopelekea makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia na makundi yanayoupinga Umoja wa Ulaya na sarafu ya pamoja Euro kuwakilishwa katika bunge la umoja huo ,hakuna chama kitakachoweza kuongoza peke yake. Muungano unahitajika. Gazeti la Cellesche Zeitung linalinganisha hali namna ilivyokuwa baada ya uchaguzi mkuu nchini Ujerumani na kuandika:"Mara baada ya uchaguzi mkuu mwezi Septemba mwaka 2013, hakuna aliyetaka kuzungumzia kuhusu muungano wa vyama vikuu - na hivi sasa neno hilo unalisikia kila mahala. Hali kama hiyo inaweza pia kutokea mjini Brussels baada ya uchaguzi wa bunge la Ulaya. Ukitupia jicho tu mgawanyo wa viti katika bunge la Ulaya utagundua kwamba wahafidhina na wasocial Democrat wanabidi washirikiane - kwa sababu peke yao wanakalia viti 403 tu toka jumla ya viti 751. Kwa namna hiyo halitozuka pia lile suala la bunge kudhibitiwa kikamilifu na makundi hayo mawili, kama hali namna ilivyo katika bunge la Ujerumani, Bundestag.

Nani Ateuliwe kuwa mwenyekiti wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya

Matokeo ya bunge la Ulaya yanabainisha mshika bendera wa chama cha kihafidhina barani Ulaya, waziri mkuu wa zamani wa Luxemburg, Jean Claude Juncker, ndiye anayestahiki kuteuliwa kuwa mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya dhidi ya spika wa bunge la Ulaya Martin Schulz wa kutoka chama cha Social Democratic cha Ujerumani SPD. Suala gazeti la "Thüringische Landeszeitung" linalojiuliza ni jee uamuzi wa wapiga kura utafuatwa?"Viongozi wa taifa na serikali za Umoja wa Ulaya wanaonyesha wamejiwekea upenu. Majina mengine yameshaanza kutajwa. Kwa sababu hakuna si Juncker na wala si Schulz anayeangaliwa na viongozi hao kuwa afadhali - kwa sababu wote wawili wanaujua kikamilifu Umoja wa Ulaya. Kama hakuna hata mmoja kati ya hao wawili atakayeteuliwa kuwa mwenyekiti wa Umoja wa Ulaya, madhara yatakuwa makubwa kwa taasisi za Umoja wa Ulaya. Kwa sababu hapo dhana za wananchi dhidi ya umangi meza katika umoja wa Ulaya zitathibitika. Na hata wale ambao hadi wakati huu wamekuwa wakiwasuta wafuasi wa makundi yanayoupinga Umoja wa Ulaya, watajikuta wameishiwa."

Angela Merkel Europapolitik Euro
Kansela Angela Merkel na nembo ya Umója wa UlayaPicha: Reuters

Matumaini Yamechomoza Ukraine

Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Ukraine ambako baada ya uchaguzi wa Jumapili iliyopita, matumaini yamechomoza ya kuketi katika meza ya mazungumzo pande zinazohasimiana. Gazeti la "Badische Zeitung" linaandika:"Si haba, Moscow na Kiev zinaonyesha utayarifu wa kuzungumza. Haitakuwa rahisi kwa pande hizi mbili kuendeleza majadiliano...Kila tukio, kila uchokozi unaweza kukorofisha mazungumzo kati ya Moscow na Kiev. Suala ni kama Proschenko ataweza kumtanabahisha Putin atambue kwamba ni kwa masilahi ya Urusi pia kama Ukraine itatulia. Ili aweze kufanikiwa atabidi kwanza kumuondoshea hofu "ndugu wa kutoka jamii ya Waslav" hawatopotelea upande wa magharibi."

Präsidentschaftswahlen in der Ukraine Poroschenko ARCHIV
Mshindi wa uchaguzi wa Ukraine PoroschenkoPicha: MYKOLA LAZARENKO/AFP/Getty Images

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Josephat Charo