Champions League : Ronaldo kurejea Old Traford
20 Desemba 2012Bayern Munich , ambayo ilifanikiwa kuingia katika fainali ya michuano hiyo msimu uliopita na kuambulia patupu dhidi ya Chelsea , London, inapambana mara hii na Arsenal London na Juventus Turin inatiana kifuani na Celtic Glasgow. Paris St Germain ambayo imetumia fedha nyingi msimu huu kununua wachezaji inakabiliana na Valencia ya Uhispania.
Lakini majaliwa ya vigogo viwili vya soka la Hispania katika upangaji wa timu zitakavyoshindana leo Alhamis katika makao makuu ya shirikisho la soka barani Ulaya UEFA , umewavutia wapenzi wengi wa soka na wote wamepambanishwa dhidi ya vilabu vikongwe vyenye uzoefu mkubwa katika soka la Ulaya.
Real Madrid , mabingwa wa sasa wa Uhispania , wamekuwa katika hali ya kukatisha tamaa katika ligi ya nchi hiyo msimu huu na wamemaliza wakiwa katika nafasi ya pili katika kundi lao na mabingwa wa Ujerumani Borussia Dortmund katika Champions League.
Ronaldo kurejea Old Traford
Lakini Ronaldo, mchezaji wa Manchester United kuanzia mwaka 2003 hadi 2009, atakuwa na hamasa kwa Real kufanya vizuri dhidi ya klabu ambayo alishinda medali ya dhahabu katika ubingwa wa Ulaya mwaka 2008.
Kocha wa Real Madrid , Jose Mourinho, ambaye aliwahi kuifunza Chelsea, pia atapambana na hasimu wake wa zamani Alex Ferguson.
"Nina hakika litakuwa pambano la pekee kwa Ronaldo" amesema Emilio Butragueno, mkurugenzi wa Real Madrid anayehusika na mahusiano ya taasisi.
"Nafikiri mashabiki watafurahi sana katika pambano hili la kufurahisha.
"Itakuwa kitu cha kufurahisha kwa kila mtu. Ningependa kucheza dhidi ya Manchester United katika sehemu za mwishoni mwa msimu huu wa champions league , lakini mashabiki wasingefurahi hata hivyo."
Manchester United mabingwa wa kombe hilo mara tatu, wamecheza na Real Madrid mara nane na kushinda mara mbili tu. Real , ambayo itaikaribisha Manchester katika mchezo wa kwanza Februari 13, iliweza kushinda mara ya mwisho kombe la Champions League mwaka 2002.
Barcelona inatisha
Barcelona hivi sasa wanapewa nafasi ya juu kulinyakua kombe hilo, licha ya kuwa wasingependa kukutana na timu yenye uzoefu mkubwa katika soka la Ulaya kama mabingwa mara saba wa kombe hilo AC Milan.
Mchezaji bora wa dunia Lionel Messi amepachika wavuni mabao 90 mwaka huu wa 2012 na ameiiwezesha Barcelona kuongoza ligi ya Uhispania kwa points tisa sasa kutoka timu inayofuatia wakati Milan wako points 14 nyuma ya Juventus Turin inayoongoza ligi ya Italia , Serie A.
Bayern Munich timu iliyonyang'anywa tonge kinywani nyumbani na Chelsea msimu uliopita inaongoza kwa points tisa katika ligi ya Ujerumani , Bundesliga. Bayern imefurahi kupangwa na Arsenal ikifahamu kuwa wapinzani wao hao wanahangaika kujiweka sawa katika ligi ya Uingereza Premier League.
Mabingwa wa Ujerumani Borussia Dortmund hawajisikii nafuu kukumbana na mabingwa wa Ukraine Shakhtar Donetsk. Mwenyekiti wa Dortmund Hans Joachim Watzke amesema haikuwa timu ambayo tungependa kukumbana nayo wakati huu. Ni timu ngumu sana lakini tumeonyesha katika mtoano katika makundi kuwa tunaweza kushinda hata timu ngumu.
Schalke 04 imepangwa dhidi ya Galatasaray ya Uturuki na Porto ya Ureno inapambana na Malaga ya Uhispania.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Yusuf Saumu