1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Champions League: nani atakayecheza katika fainali ya Lisbon?

28 Aprili 2014

Timu zitakazocheza fainali ya Champions League zitajulikana wiki hii, wakati Bayern Munich ikijaribu kupambana katika mchuano wa marudiano wa nusu fainali baada ya kushindwa goli moja kwa sifuri na Real Madrid

https://p.dw.com/p/1Bpkj
Champions League Real Madrid Bayern München
Picha: Reuters

Chelsea pia italenga kumaliza kazi mjini London, baada ya kutoka sare ya kutofungana goli ugenininan Atletico Madrid. Bayern wanawaalika Real kesho Jumanne uwanjani Allianz Arena, wakifahamu wazi kuwa baada ya kushindwa kubusu nyavu za mpinzani wake ugenini mjini Madrid, wanaweza kuwa na mpambano mgumu wa marudiano.

Ushindi wao wa Jumamosi katika Bundesliga dhidi ya Werder Bremen uliwapa motisha kwa kufunga magoli matano lakini nao wakafungwa mawili katika njia ambayo huenda ilisababisha tabasamu kubwa mjini Madrid. Frank Ribery ni mmoja wa wachezaji wa Bayern watakaotegemewa sana kuisumbua safu ya ulinzi ya Real, jinsi anavyosema nahodha wake Phillip Lahm "Sina wasiwasi kumhusu Frank Ribery. Frank ni mchezaji hodari ambaye anayeweza kuamua hatima ya timu na leo amefunga bao tena. Nadhani pia atafunga tena kesho Jumanne, hilo nategemea, lakini pia kama mtu mwingine ataeza kufanya hivyo tutakuwa na nafasi kubwa zaidi ya kutinga fainali".

Real Madrid wanaingia Munich wakijipiga kifua baada ya ushindi wao wa magoli manne kwa sifuri dhidi ya Osasuna katika Laliga mwishoni mwa wiki. Na mmoja wa wachezaji watakaokuwa mwiba kwa upande wa lango la Bayern, Cristiano Ronaldo, maarufu kama CR7 alifunga magoli mawili ya kiufundi katika mechi hiyo ya Osasuna.

Chelsea watalenga kumalizia kazi dhidi ya Atletico Madrid
Chelsea watalenga kumalizia kazi dhidi ya Atletico MadridPicha: Peter Parks/AFP/Getty Images

Nao majirani wao Atletico Madrid pia wana motisha kubwa kabla ya ziara yao mjini London kumyenanya na Chelsea, kwa sababu mchuano wa kwanza uliishia sare tasa. Vijana hao wa Diego Simeone walipata ushindi wao wa nane mfululizo katika La Liga hapo jana, goli moja kwa sifuri ugenini kwa Valencia, matokeo ambayo yamewaacha tu na mechi mbili ambazo wakishinda wanavikwa taji la Uhispania.

Chelsea ambao jana wamewashinda Liverpool magoli mawili kwa sifuri wana masaibu chungu nzima kikosini. Mlinda lango Petr Cech yuko mkekani, na glovu zake zimevaliwa na Mark Schwarzer. John Terry ana jeraha pia. Frank Lampard na John Obi Mikel wanatumikia adhabu, wakati Nemanja Matic na Mohammed Salah hawaruhusiwi kucheza dimba hilo. Eden Hazard haijulikani kama atakuwa amepona vizuri jeraha lake, wakati naye Samuel Eto'o akiwa mkekani pia.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman