Champagne kuwania urais wa FIFA
23 Oktoba 2015Champagne mwenye umri wa miaka 57 amesema ana uungwaji mkono kutoka kwa mataifa matano wanachama wa FIFA. Naibu huyo katibu mkuu wa zamani wa FIFA ndiye mgombea wa nne rasmi katika uchaguzi huo, ambao umepangwa kufanyika Februari 26.
Wapinzani wake waliothibitisha kushiriki ni Rais wa Shirikisho la Kandanda Ulaya – UEFA Michel Platini, Mwanamfalme Ali bin al Hussein wa Jordan na aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Trinidad and Tobago David Nahkid, ijapokuwa majina mengine huenda yakaibuka kabla ya muda wa mwisho wa siku ya Jumatatu.
Uchaguzi wa kumrithi Blatter, ambaye amekuwa rais wa FIFA tangu mwaka wa 1998 na ambaye anajiuzulu, unakuja katika wakati ambapo kuna mgogoro katika shirikisho hilo la kandanda la kimataifa.
Waendesha mashtaka wanawachunguza maafisa wakuu wa FIFA, wakiwemo Blatter na Platini, kama sehemu ya upelelezi mpana kuhusu ufisadi na rushwa katika shirikisho hilo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri:Yusuf Saumu