Chama tawala Uturuki AKP chashinda katika chaguzi
31 Machi 2014Akiwahutubia wafuasi wake kutoka ubaraza wa ghorofani wa makao makuu ya chama cha AKP mjini Istanbul baada ya ushindi katika chaguzi za serikali za mitaa,Erdogan ameapa kukabiliana na wapinzani wake ambao wamemshutumu kuhusika katika ufisadi na kuvujisha siri za serikali.
Erdogan ambaye kashfa hizo zimekuwa changamoto kubwa kuwahi kumkumba katika utawala wake wa miaka 12 amewataja wapinzani wake kuwa magaidi na washirika wa maovu.
Hotuba hiyo ya waziri mkuu huyo wa Uturuki ni tofauti na za miaka ya nyuma ambazo zilikuwa za kuhimiza maridhiano miongoni mwa pande tofauti katika safu ya kisiasa na kipindi hiki hotuba yake inadokeza kuchukuliwa kwa hatua kali dhidi ya wapinzani wake baada ya kunyakua ushindi katika uchaguzi huo muhimu kwa chama tawala.
Erdogan aapa kukabiliana na maadui wake
Kipindi cha kampeni kabla ya uchaguzi huo hapo jana,kilishuhudia hali ya vuta nikuvute kati ya Erdogan na mpinzani wake Fethullah Gulen ambaye anashutumiwa kwa kutumia maafisa kadhaa katika idara ya polisi na mahakama kutunga kashfa za ufisadi katika njama ya kumuangusha madarakani Erdogan.
Erdogan amewafuta kazi maelfu ya polisi,majaji na waendesha mashitaka tangu kuanzishwa kwa uchunguzi wa madai ya visa vya ufisadi yanayohusisha wafanyabiashara,wanawe na mawaziri walio karibu naye.
Mzozo huo uliwatia wasiwasi wawekezaji nchini humo na kuporomosha thamani ya sarafu ya Uturuki, Lira ,kuanzia mwezi Januari na kusababisha hasara katika masoko ya hisa.
Imani ya wawekezaj yarejea baada ya uchaguzi
Hata hivyo ushindi wa AKP umeashiria muendelezo wa uongozi wa kisiasa na kurejesha kwa kiasi fulani imani ya wawekezaji.Hii leo thamani ya Lira ilipanda katika kiwango ambacho hakijashuhudiwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita.
Kufikia leo asubuhi, asilimia 98 ya kura zilikuwa zimehesabiwa na AKP ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 2002,kilikuwa kinaongoza kwa asilimia 45.6 huku chama cha upinzani cha CHP kikifuata kwa asilimia 28 ya kura zilizohesabiwa.
Wachambuzi nchini Uturuki wanahofia kuwa Erdogan ambaye katika siku za hivi karibuni ameonekana kunoa makali zaidi katika kukabiliana na wapinzani wake ataongeza mbinyo dhidi ya anaowaona maadui zake kisiasa baada ya kuapa kukabiliana nao katika hotuba yake hiyo.
Tayari mapema mwaka huu alizifunga shule za mpinzani wake Gulen, ambaye wakati mmoja alikuwa mshirika wake kisiasa,ameifunga mitandao ya kijamii ikiwemo twitter na youtube hatua ambayo imeshutumiwa vikali na nchi za magharibi na kuvikandamiza vyombo vya habari.
Ushindi huo katika chaguzi za serikali za mitaa huenda ukampa Erdogan msukumo wa kugombea katika uchaguzi wa rais unaotarajiwa mwezi Agosti mwaka huu au kuamua kuwania kwa muhula wa nne wadhifa wa waziri mkuu katika uchaguzi wa bunge mwaka ujao ili kuendeleza utawala wake, kama Waziri mkuu.
Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Dpa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman