CCM yapata ushindi mnono uchaguzi wa serikali za mitaa
29 Novemba 2024Uchaguzi wa serikali za mitaa nchini Tanzania uliofanyika Jumatano ulionekana kama mtihani muhimu kwa taasisi za kidemokrasia za nchi hiyo kuelekea uchaguzi wa urais mwaka ujao, lakini ulighubikwa na madai ya udanganyifu na matukio ya vurugu.
Chama kikuu cha upinzani Chadema kimesema kuwa wanachama wake watatu waliuawa katika matukio yanayohusiana na uchaguzi huo. Tanzania ilikuwa inachagua zaidi ya viongozi 80,000 wa mitaa wenye mamlaka makubwa.
Matokeo rasmi yalionyesha kuwa chama cha CCM cha Rais Samia Suluhu Hassan kilishinda zaidi ya asilimia 98, huku vyama vingine 18 vikigawana viti vilivyobaki.
Waziri wa Nchi anaehusika na tawala za mikoa na serikali za mitaa, Mohamed Mchengerwa, aliyesimamia uchaguzi huo, alisema viongozi hao waliochaguliwa wanapaswa kuapishwa mara moja.
Huu ulikuwa mtihani wa kwanza kwa Rais Samia kwenye sanduku la kura kabla ya uchaguzi wa urais na ubunge Oktoba mwaka ujao.
Chadema Alhamisi ilisema imeitisha mkutano wa dharura Ijumaa kujadili uchaguzi huo na kutoa tamko kuhusu uchaguzi baada ya mkutano.
Soma pia: Watanzania washiriki uchaguzi wa serikali za mitaa
Pia ilipinga wiki iliyopita kuhusu kile ilichokiita kuondolewa kwa wagombea wake kwa njia isiyo ya haki. Tanzania, taifa lenye watu milioni 61, limekuwa likijulikana kama moja ya demokrasia thabiti zaidi barani Afrika.
CCM na mtangulizi wake TANU wameshikilia madaraka tangu uhuru mwaka 1961, lakini kimekuwa kikilaumiwa kwa ukandamizaji mkubwa kuelekea uchaguzi huo.
Samia alichukua madaraka baada ya kifo cha ghafla cha mtangulizi wake mwenye mkono wa chuma, John Magufuli, mwaka 2021. Awali alipongezwa kwa kulegeza masharti aliyoweka Magufuli dhidi ya upinzani na vyombo vya habari.
Hata hivyo, makundi ya haki za binadamu na serikali za Magharibi zimeikosoa CCM kwa kile wanachokiona kama ukandamizaji mpya kuelekea uchaguzi, huku wanasiasa wa upinzani wakikabiliwa na kukamatwa mara kwa mara, utekaji nyara na mauaji.
Kanisa Katoliki Alhamisi lilikemea vurugu hizo, likisema nchi inapitia kipindi kigumu kilichojaa maumivu na mateso.
"Hili ni jambo baya, lakini kwa bahati mbaya hatuoni likilaaniwa vikali," alisema Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa'ichi.
Upinzani ulisusia uchaguzi wa mwaka 2019 kwa madai ya vurugu na vitisho, hali iliyosababisha ushindi mkubwa wa CCM.