1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama tawala nchini Zimbabwe, chataka awamu ya pili ya uchaguzi wa Rais.

Nyanza, Halima3 Aprili 2008

Wakati matokeo ya uchaguzi wa bunge la Zimbabwe, yakionesha kuwa chama cha upinzani cha MDC kimeshinda viti 99, na chama tawala cha ZANU PF kimeshinda viti 97, Chama tawala kinataka kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi

https://p.dw.com/p/DbEa
Robert Mugabe wa Zimbabwe, ambaye chama chake kinataka awamu nyingine ya uchaguzi wa Rais nchini humo.Picha: picture-alliance/ dpa

Wakati hali ikiwa hivyo, Chama tawala kinachoongozwa na Rais Robert Mugabe kimesema kiko tayari kuingia tena katika duru ya pili ya uchaguzi kati ya kiongozi wake na mpinzani wake Morgan Changirai.

Naibu Waziri wa Habari wa nchi hiyo, Bright Matonga amesema ZANU PF iko tayari kurudia tena uchaguzi huo.

Aidha amesema, Rais Mugabe ambaye hajaonekana hadharani tangu alipopiga kura yake Jumamosi iliyopita ni mzima wa afya na anasubiri matokeo.

Aidha, Tume ya Taifa ya uchaguzi nchini humo imesema chama tawala cha ZANU PF kinachoongozwa na Rais Mugabe kimeshindwa kudhibiti nafasi bungeni kwa mara ya kwanza katika kipindi cha karibu miongo mitatu.

Chama cha upinzani cha Movement for Democratic Change -MDC-, kimedai kuwa Rais Mugabe anaonekana pia kupoteza kura za kiti hicho cha urais na hivyo anapaswa kukubali kushindwa kwake.

Habari zinasema kuwa wasaidizi wa Rais Mugabe, wamekasirishwa na na madai yanayotolewa na chama cha upinzani cha MDC, kwamba wameshinda uchaguzi, hali ambayo wanaweza kuadhibiwa kwa hilo.

Mmoja wa wanasiasa waandamizi wa chama tawala cha ZANU PF, Christpha Mutsvanga amesisitiza kuwa tume ya uchaguzi nchini humo ndiyo yenye uhalali wa kutangaza matokeo ya uchaguzi na si vinginevyo.

Amesema wao ZANU PF wanafanya kazi tu na chombo halali kisheria kinachosimamia uchaguzi, ambayo ni tume ya uchaguzi ya Zimbabwe, na wanasubiri mpaka hapo itakapotamka yenyewe uamuzi wa mwisho wa matokeo hayo na kwamba hawatasikiliza mtu au taasisi yoyote ambayo haina ruhusa kisheria kuzungumzia suala hilo.

Lakini kwa upande wao, upinzani nchini humo wamekuwa wakishinikiza Rais Mugabe akubali kushindwa kutokana na kudai kwamba matokeo yanaonesha hivyo na kulaumu kampeni zinazofanywa vyombo vya habari vya serikali iliyo madarakani kwamba vinawajenga watu kuona kwamba chama chao hakikushinda katika uchaguzi huo, kama anavyosisitiza Katibu mkuu wa chama hicho cha MDC Tendai Biti

Aidha wamepinga hatua ya kufanyika tena kwa awamu ya pili ya uchaguzi huo wa Rais.

Amesema matokeo ya viti waliyopata yanaonesha wazi kwamba wameshinda uchaguzi huo bila ya hata kuingia katika duru hiyo ya pili.

Amelaumu pia ripoti zinazotolewa na vyombo vya serikali kwa kudai kuwa inawaandaa watu kuhusiana na uchaguzi huo wa duru ya pili.

Mvutano huo kuhusiana na matokeo ya uchaguzi nchini Zimbabwe unakuja wakati nchiyo ikikabiliwa na matatizo makubwa kiuchumi, hususan kutokana na kwamba Zimbabwe inakabiliwa na vikwazo vya kiuchumi iliyowekewa na nchi hza magharibi.