Chama tawala Ethiopia chashinda kwa kishindo
25 Mei 2010Maelfu ya wafuasi wa chama tawala nchini Ethiopia wamemiminika katika eneo la uwanja mkuu mjini Addis Ababa leo wakishangiria ushindi wa waziri mkuu Meles Zenawi katika uchaguzi uliofanyika kwa amani na kupuuzia madai ya upande wa upinzani na makundi ya haki za binadamu ya wizi wa kura.
Wakipepea bendera ya Ethiopia , wakivalia fulana za chama tawala pamoja na kofia, huku wakiwa wameshika picha ya Meles Zenawi juu, waungaji mkono wa chama tawala waliimba, heshimuni matokeo ya uchaguzi, heshimuni uamuzi wetu, heshimuni chaguo letu.
Serikali ya nchi hiyo ambayo ni mshirika mkubwa wa Marekani katika eneo hilo imeonya kuwa mwanasiasa yeyote ambaye atajaribu kuzusha ghasia za baada ya uchaguzi atawajibishwa. Viongozi wa upinzani waliwekwa ndani kwa wingi baada ya ghasia zilizomwaga damu kufuatia ushindi wa Meles mwaka 2005.
Kiongozi wa ngazi ya juu wa upinzani Beyene Petros ameshutumu matokeo ya mwanzo yaliyotolewa na tume ya uchaguzi ya taifa, lakini hakueleza ni hatua gani itakayochukuliwa na chama chake.
Ushindi unaweza kutangazwa tu kwa kuwa kumefanyika udanganyifu, na sio kinyume chake.
Mabango yaliyochapishwa katika rangi za bendera ya taifa ya kijani, njano na nyekundu yaligawiwa wakati watu wakijikusanya katika uwanja mkuu wa jiji la Ethiopia, Addis Ababa wa Meskel , kusherehekea ushindi wa kishindo alioupata mpiganaji huyo wa zamani wa chini kwa chini , mabango mengi yakiwa yamendikwa kwa lugha ya Kiingereza pamoja na lugha ya Kiamharik. Baadhi ya mabango yalikuwa na maandishi yanayosema, kura zetu haziuzwi, acheni kututilia shaka, heshimuni kura zetu halali, tunamchagua kiongozi wetu na sio mwingine.
Matokeo yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi jana Jumatatu yanaonyesha kuwa chama tawala nchini Ethiopia cha Ethiopia Peoples Revolutionary Democratic Front , EPRDF, na washirika wake wameshinda wingi mkubwa wa kura katika majimbo tisa kati ya kumi na moja pamoja na miji.
Chama cha EPRDF kimeusambaratisha muungano wa vyama vinane vya upinzani unaofahamika kama Medrek katika jimbo la Oromia, jimbo ambalo lina wakaazi wengi na ambalo kimsingi lilikuwa ngome ya upinzani.
Kiongozi wa ujumbe wa umoja wa Ulaya unaoangalia uchaguzi huo Thijs Berman amesema kuwa wamepokea malalamiko kadha kutoka kwa upande wa upinzani.
Tumepokea malalamiko kadha, na tunajaribu kufanya uchunguzi kuona iwapo ni makubwa kiasi gani yameenea kwa kiasi gani, na hatuwezi hadi sasa kusema lolote kuhusu suala hilo.
Ujumbe wa umoja wa Ulaya unaoangalia uchaguzi huo , umesema kuwa utatoa ripoti yake kuhusu uchaguzi huo leo Jumanne.
Waziri mkuu Meles Zenawi aliwasili katika uwanja unaofanyika sherehe hizo katikati ya jiji la Addis Ababa asubuhi ya leo na aliwahutubia wafuasi wake kwa lugha ya Kiamhara wakati wanajeshi waliovalia sare zao za buluu wakiwa katika doria.
Mwandishi: Ludger Schadomsky/ ZR/ Sekione Kitojo.
Mhariri: Abdul-Rahman