1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha wanasheria Tanganyika chaonya dhidi ya uchochezi

Veronica Natalis9 Septemba 2019

Chama cha wanasheria Tanganyika kimeonya kuwa kauli zinazochochea watu kujichukulia sheria mikononi mwao ni uvunjifu wa sheria, na viongozi wanaofanya hivyo wanastahili kuchukuliwa hatua za kisheria.

https://p.dw.com/p/3PGsg
Tansania Wahlkampf - UKAWA
Picha: Getty Images/AFP/D. Hayduk

Chama cha wanasheria Tanganyika TLS kimewaonya viongozi wa siasa nchini Tanzania wanaotoa kauli zinazochochea watu kujichukulia sheria mkononi mwao, kikisema hayo ni kinyume cha sheria na viongozi hao wanapaswa kushitakiwa. Hayo yanajiri wakati kukishuhudiwa baadhi ya viongozi wa siasa na serikali nchini humo wakitamka hadharani kauli zinazoashiria kuwapiga watu na kuwavunja miguu.

Katika mkutano mkuu wa nusu mwaka wa chama cha wanasheria Tanganyika TLS, uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa AICC uliopo Arusha, kaskazini mwa Tanzania, Rais wa TLS Dk. Rugemeleza Nshalla amesema ni kosa la kisheria kwa kiongozi au mwananchi yeyote kutekeleza au kutoa kauli inayohamasisha watu kujichukulia sheria mkononi. Ameongeza kuwa ni mahakama pekee yenye mamlaka ya kutoa adhabu na mtu yeyote anayetamka au kuchochea vitendo hivyo anatakiwa kuchukuliwa hatua za kisheria.

Hivi karibuni kumekuwa kukishuhudiwa matamko mbalimbali ya viongozi wa serikali na siasa nchini Tanzania, matamko yanayotoa tafsiri ya kuchochea vitendo vya kujichukulia sheria mkononi.

Kongamano katika chuo kikuu cha Da es Salaam kujadili masuala ya siasa na uchumi Tanzania. (Picha ya maktaba)
Kongamano katika chuo kikuu cha Da es Salaam kujadili masuala ya siasa na uchumi Tanzania. (Picha ya maktaba)Picha: DW/G. Njogopa

Miongoni mwa kauli hizo ni ile iiliyotolewa na mkuu wa wilaya ya Kigamboni jijini Dar es salaam Sarah Msafiri wakati akihojiwa na chombo kimoja cha habari alisema kuwa vibaka watakaokamatwa katika wilaya yake watapigwa na kuvunjwa miguu kwani wakipelekwa mahakamani watapatiwa dhamana.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine unatoa mwelekeo na kuangalia hali ya utawala wa kisheria nchini Tanzania. Aidha Rais wa TLS pia, ameonya kuwa ni kosa la kisheria kuingiliwa kwa mawasiliano ya mawakili kwa sababu sheria inakataza mawasiliano ya wakili na mteja kuchukuliwa na kuchapishwa popote pale.

Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo mgeni rasmi jaji mkuu mstaafu wa mahakama ya Kenya Dr. Willy Mutunga amesisitiza suala la upatikanaji wa haki sawa za kisheria kwa wananchi wote kwani hakuna aliye juu ya sheria. Mkutano huo umehudhuriwa na mawakili takribani elfu tatu kutoka mikoa yote ya Tanzania bara. Veronica Natalis DW,Arusha.