Chama cha upinzani Zimbabwe kimejitangazia ushindi wa urais
2 Aprili 2008Upande wa upinzani nchini Zimbabwe unadai umeshinda uchaguzi mkuu wa mwishoni mwa juma lakini chama tawala cha ZANU-PF kimeyaita madai hayo kama ndoto.
Hali halisi haieleweki kutokana na tume ya uchaguzi kuwa hadi sasa haijatoa matokeo.
Chama cha upinzani cha Movement For Democratic change,MDC cha Morgan Tsvangirai katika mkutano kilichouitisha mjini Harare jumatano kimedai kuwa kimeshinda uchaguzi huo na mtetezi wao ndie ameibuka mshindi .Madai hayo yametolewa na katibu mkuu wa chama hicho Tenda Biti.Aidha ameimtaka Bw Mugabe akubali matokeo.
Lakini serikali imelaani hatua hiyo ya chama cha MDCya kudai ushindi bila ya kusubiri matokeo ya tume ya uchaguzi. Naibu waziri wa habari Bright Matonga ameyaita madai ya MDC kama ndoto na kuongeza kuwa hatua ya chama cha upinzani ilikuwa na nia ya kuchokoza jeshi.Ameendelea kuwa MDC inacheza mchezo wa kitoto tena mbaya.Pia akaonya upande wa upinzani dhidi ya kutaka kufanya kama kile kilichotokea Kenya mapema mwaka huu.Naibu waziri amesema kuwa chama hicho kingesubiri matokeo yatakayotolewa na tume ya uchaguzi.
Waziri wa mashauri ya kigeni wa Uingereza,David Milliband,akilihutubia bunge la Uingereza leo jumatano ameilaani tume ya uchaguzi ya Zimbabwe kwa kuchelewesha kutoa matokeo ya urais akisema kuwa inajua matokeo lakini inafanya makusudi kuyakalia.
Hadi kufikia sasa matokeo ya uchaguzi wa urais yalikuwa hayajatangazwa.Yeye waziri mdogo wa habari ameitetea tume ya uchaguzi kuwa haijafanya kosa lolote kuchelewa kutoa matokeo.Amesema kuwa sheria zinaipa tume mda wa situ sita kuanzia siku ya kupiga kura kuweza kutoa matangazo.Hii ina maana kuwa matokeo yanaweza yasitolewe hadi ijumaa.
Ameongeza kuwa hawatashinikizwa na yeyote yule na pia kuwa Mugabe haendi popote.
Lakini katika ubunge inaonekana upinzani unaongoza jambo ambalo halijapingwa na upande wa serikali.
Upinzani kwa pamoja umeshinda viti 105 huku chama cha rais Mugabe cha ZANU PF kikipata viti 93.Ikiwa matokeo hayo yatathibitishwa na tume ya uchaguzi ambayo imesema itayatoa yote jumatano jioni,itamaanisha kuwa chama cha ZANU-PF kimepoteza wingi wa viti bungeni.Na hii itakuwa mara ya kwanza chama cha MDC kupata wingi wa viti bungeni.Hata hivyo mamlaka kamili yako mikononi mwa raisi.
Hali hii ya kuchanganyikiwa itaondolewa tu ikiwa habari kamili zitatolewa na tume ya uchaguzi.