Chama cha UDPS chamfukuza na kumtenga mwenyekiti wake
31 Januari 2022Hatua ya kumfukuza na kumtenga Jean-Marc Kabund kutoka UDPS imechukuliwa wiki mbili, baada ya yeye mwenyewe kutangaza kupitia ukurasa wake wa Twitter, kujiuzulu kutoka wadhifa wake wa makamu wa kwanza wa Spika wa Bunge la Kitaifa.
Hata hivyo, hadi sasa bado hajatekeleza hatua hiyo lakini wawakilishi wa chama bungeni pamoja na muungano wa taifa unaomuunga mkono Rais Félix Tshisekedi tayari wamemtaka aondoken katika wadhifa huo.
Soma pia: Mahakama ya Congo yatupa ombi la Kabila kujitetea mahakamani
Hatua ya kumfurusha na kumtenga Jean-Marc Kabund ilisomwa na Victor Wakwenda, kiongozi wa tume ya demokrasia katika chama (CDP).
"Kufuatana na uzito wa makosa aliyoyafanya, tume ya Kitaifa ya Nidhamu iliamua kumpokonya Bwana Jean-Marc Kabund majukumu yake yote ndani ya UDPS na kumtenga na chama hiki," alisema Wakwenda.
Aidha, tume ya kidemokrasia ya UDPS imeunda bodi ya kitaifa kwa ajili ya usimamizi wa chama hicho tawala, bodi hiyo Inaundwa na Victor Wakwenda ambae ni Kiongozi wa tume hiyo, Jacqemain Shabani, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ya chama, pamoja na Augustin Kabuya ambae ni katibu mkuu wa UDPS na ndiye sasa anachukua nafasi ya Jean-Marc Kabund kama mkuu wa chama hicho.
Soma pia: Upinzani DRC wadai Tshisekedi anaandaa ushindi wa uchaguzi
"Tunaamini kwamba bodi hii ya utendaji itafanya vyema zaidi ikiwa tu Bwana Augustin Kabuya ambaye anafaidika na kuondolewa kwa Kabund, ataachana na dhuluma za zamani, akiweka kando kila kitu ambacho raia wamekilalamikia. Halafu bodi hii inaweza kumrahisishia rais wa nchi kupata muhula wa pili," alisema Jean-Pierre Mulemangabo, mchambuzi huru wa kisiasa.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inatarajiwa kufanya uchaguzi wake Novemba 2023. Rais Félix Tshisekedi tayari ametangaza kuwania muhula wa pili. Lakini wapinzani wake wanamtuhumu kuidhibiti tume huru ya taifa ya uchaguzi (CENI) pamoja na korti ya Katiba.